Hamia kwenye habari

VIJANA HUULIZA

Viapo vya Ubikira

Viapo vya Ubikira

 Kiapo cha ubikira ni nini?

 Kiapo cha ubikira ni ahadi ya kutofanya ngono kabla ya kufunga ndoa ambayo mtu hutoa kwa njia ya maandishi au maneno.

 Viapo vya ubikira vilipata umaarufu katika miaka ya 1990 wakati kanisa la Southern Baptist Convention nchini Marekani lilianzisha kampeni yenye kichwa “True Love Waits” (Upendo wa Kweli Husubiri). Katika kampeni hiyo vijana walitiwa moyo wakatae kufanya ngono kabla ya ndoa wakichochewa na kanuni za Biblia na pia vijana wenzao.

 Kampeni nyingine kama hiyo ilianzishwa muda mfupi baadaye na ilihusisha matukio mbalimbali. Wahudhuriaji ambao walikula kiapo walipewa pete ya fedha iliyoonyesha (na kuwakumbusha) msimamo wao wa kutofanya ngono kabla ya ndoa.

 Je, viapo vya ubikira vina faida?

 Jibu la swali hilo linategemea yule unayemuuliza.

  •   Kulingana na watafiti Christine C. Kim na Robert Rector, “uchunguzi mwingi unaonyesha kwamba viapo vya ubikira vimefanya vijana wasifanye ngono mapema au vimepunguza kasi ya vijana kufanya ngono.”

  •   Kulingana na utafiti uliochapishwa na Taasisi ya Guttmacher, uchunguzi unaonyesha kwamba “kuna uwezekano kwa vijana wanaokula ‘viapo vya ubikira’ kufanya ngono sawa tu na wale ambao hawajala kiapo.”

 Kwa nini matokeo ya utafiti yanapingana?

  •   Baadhi ya utafiti hulinganisha wale waliokula viapo na wasioapa ambao wana maoni tofauti kuhusu ngono.

  •   Utafiti mwingine hulinganisha wale waliokula viapo na wasioapa ambao wana maoni yanayofanana kuhusu ngono.

 Utafiti wa aina hiyo ya pili umefunua nini? Daktari Janet Rosenbaum, mtaalamu wa afya ya vijana, anasema kuwa baada ya miaka mitano, “waliokula viapo na wasiokula viapo hawatofautiani katika vitendo vya ngono.”

 Njia nzuri zaidi

 Kampeni za viapo vya ubikira zimeanzishwa kwa nia njema. Tatizo ni kwamba katika kampeni hizo vijana hawapewi kanuni zitakazowasaidia waendelee kufanya hivyo hadi mwisho. Wengi wanaoahidi kuendelea kuwa mabikira “hawatimizi kiapo chao,” anasema Daktari Rosenbaum. “Kuepuka kufanya ngono kunapaswa kuwa azimio la mtu na si jambo ambalo linafanywa kwa sababu ya kushiriki katika kampeni fulani.”

 Biblia inawahimiza watu waweke maazimio kama hayo, si kupitia viapo vya maneno au maandishi, bali kwa kuwasaidia ‘watumie nguvu zao za ufahamu ambazo zimezoezwa kutofautisha yaliyo sawa na yaliyo makosa pia.’ (Waebrania 5:​14) Zaidi ya yote, kuwa bikira hakumsaidii tu mtu aepuke magonjwa na mimba, badala yake ni njia ya kumheshimu Mwanzilishi wa ndoa.​—Mathayo 5:​19; 19:​4-6.

 Viwango vilivyowekwa katika Biblia vinatunufaisha. (Isaya 48:17) Watu wote​—bila kujali umri wao​—wanaweza kusitawisha uwezo wa kutii amri ya Mungu ya ‘kuukimbia uasherati.’ (1 Wakorintho 6:​18) Hivyo watakapofunga ndoa, wataweza kufurahia mahusiano ya ngono, bila wasiwasi au majuto yanayowapata wale wanaofanya ngono kabla ya ndoa.