Hamia kwenye habari

VIJANA HUULIZA

Mitandao ya Kijamii Inaniathirije?

Mitandao ya Kijamii Inaniathirije?

 Je, wazazi wako wanakuruhusu kutumia mitandao ya kijamii? Ikiwa wanakuruhusu, makala hii itakusaidia kufikiria mambo matatu muhimu.

Kwenye ukurasa huu

 Mitandao ya kijamii inaathirije jinsi ninavyotumia muda wangu?

 Kutumia mitandao ya kijamii ni kama kupanda farasi mwenye nguvu—usipomwongoza, yeye ndiye atakayekuongoza wewe.

 “Ninapoingia kwenye mtandao wa kijamii ninajiambia nitaangalia kwa ‘dakika chache tu,’ lakini baadaye ninakuja kushtukia kwamba saa kadhaa zimepita! Ni rahisi kuwa mraibu wa mitandao ya kijamii na inapoteza muda mwingi.”​—Joanna.

 Je, wajua? Mitandao ya kijamii imekusudiwa kuwafanya watu wawe waraibu wa kuitumia. Watu waliobuni mitandao hiyo wanajua kwamba watapata pesa nyingi zaidi kutokana na matangazo iwapo mtandao wa kijamii utawavutia watu wengi na watatumia muda mrefu humo.

 Jiulize: ‘Je, ninapoteza muda mwingi nikiangalia-angalia mambo ambayo yamewekwa kwenye mitandao ya kijamii bila kujua? Je, ninaweza kutumia sehemu ya muda huo kufanya mambo yenye manufaa zaidi?’

 Unachoweza kufanya. Jiwekee mipaka ya muda utakaotumia kwenye mitandao ya kijamii, na uheshimu mipaka hiyo.

Jiwekee mipaka ya muda utakaotumia kwenye mitandao ya kijamii

 “Niliweka muda hususa kwenye simu yangu ili baadhi ya programu zijifunge baada ya muda huo kwisha. Mwanzoni nililazimika kujidhibiti sana, lakini baadaye nilipata usawaziko, nilitumia mitandao ya kijamii lakini sikupoteza muda wangu.”​—Tina.

 Kanuni ya Biblia: “[Tumieni] vizuri kabisa wakati wenu.”​—Waefeso 5:16.

 Mitandao ya kijamii inaathirije usingizi wangu?

 Wataalamu wengi wanasema kwamba matineja wanahitaji kulala angalau saa nane, lakini wengi wao wanalala saa chache. Jambo moja linalochangia tatizo hilo ni matumizi ya mitandao ya kijamii.

 “Mimi huangalia simu yangu kabla ya kulala lakini nakuja kugundua kwamba nimepoteza saa nyingi nikiangalia-angalia mambo ambayo watu wameweka mitandaoni. Hilo ni zoea baya na ninajitahidi kuliacha.”​—Maria.

 Je, wajua? Mtu anapokosa usingizi wa kutosha anaweza kuwa na wasiwasi mwingi na hata kushuka moyo. Jean Twenge, ambaye ni profesa wa saikolojia anasema kwamba kukosa usingizi kunafanya watu wengi wanahisi hawana furaha. Isitoshe, anasema kwamba mtu asipopata usingizi wa kutosha “kwa muda mrefu” anaweza kupata “matatizo makubwa ya kiakili.” a

 Jiulize: ‘Mimi hulala kwa saa ngapi kila siku?’ ‘Je, ninaangalia-angalia vitu kwenye mitandao ya kijamii badala ya kupumzisha akili ili kujiandaa kulala?’

 Unachoweza kufanya. Ondoa vifaa vya kielektroni kwenye chumba chako cha kulala usiku. Hali inaporuhusu, epuka kutazama skrini angalau saa mbili kabla ya kulala. Ikiwa unahitaji saa ya kukuamsha jaribu kutumia saa nyingine, badala ya saa iliyo kwenye simu au tablet.

Epuka kutumia mitandao ya kijamii kwa muda fulani kabla ya kulala

 “Wakati mwingine ninachelewa kulala kwa sababu ya kutumia kifaa changu muda mrefu, lakini ninajitahidi kurekebisha tatizo hilo. Ninahitaji kuacha tabia za kitoto na kuwa mtu mwenye kuwajibika zaidi. Ninahitaji kulala mapema ili siku inayofuata niwe na nguvu za kutekeleza majukumu yangu.”​—Jeremy.

 Kanuni ya Biblia: “[Hakikisha] mambo muhimu zaidi.”​—Wafilipi 1:10.

 Mitandao ya kijamii inaathirije hisia zangu?

 Katika utafiti mmoja, karibu nusu ya wasichana walio sekondari ambao walishiriki katika utafiti huo walisema kwamba “muda mwingi wanakuwa na huzuni na wanahisi kwamba wamekata tamaa.” Mitandao ya kijamii inachangia hali hiyo. Dakt. Leonard Sax anasema hivi: “Unapotumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii ukijilinganisha na wengine unaongeza uwezekano wa kushuka moyo. b

 “Kwa kawaida vijana hujilinganisha na wengine, na mitandao ya kijamii hufanya iwe rahisi zaidi kufanya hivyo. Unaweza kutumia saa nyingi kuangalia picha ambazo watu wameweka kisha ukaanza kulinganisha maisha yako na yao, au unaweza kutazama jinsi marafiki wako wanavyojifurahisha na kuhisi kwamba wewe hufurahii maisha kama wanavyofanya.”​—Phoebe.

 Je, wajua? Ingawa mitandao ya kijamii inaweza kukusaidia kuwasiliana na marafiki wako, bado kuna umuhimu wa kuwa na mazungumzo ya uso kwa uso. Dakt. Nicholas Kardaras aliandika hivi: “Tunapata furaha zaidi tunapowasiliana na watu moja kwa moja kuliko tunapotumia vifaa vya kielektroni. Kuwasiliana kupitia vifaa vya kielektroni hakutoshelezi uhitaji tulio nao wa kuwa na mawasiliano yenye kina, kutoka moyoni.” c

 Jiulize: ‘Je, ninajihisi mpweke baada ya kuangalia mambo ambayo marafiki wangu wanafanya?’ ‘Je, ninahisi maisha yangu si yenye kusisimua kama ya marafiki wangu wanaoweka picha mtandaoni?’ ‘Je, ninahisi vibaya ninapogundua kwamba nilichoweka mtandaoni hakijapewa “alama ya kidole gumba” au likes?

 Unachoweza kufanya. Jaribu kuacha kutumia mitandao ya kijamii kwa siku kadhaa, juma moja, au hata mwezi mmoja. Tumia muda mwingi zaidi pamoja na marafiki wako uso kwa uso au uzungumze nao kwenye simu. Huenda ukaona kwamba kufanya hivyo kunakusaidia kupunguza mkazo na kuhisi ukiwa na furaha zaidi.

Je, unaweza kutumia muda mwingi zaidi pamoja na marafiki wako uso kwa uso?

 “Nilitambua kwamba nilipokuwa nikitumia mitandao ya kijamii nilitamani sana kujua mambo ambayo watu walikuwa wakifanya. Baada ya kufuta akaunti zangu, nilihisi kana kwamba nimetua mzigo mkubwa na sasa hata nimepata muda mwingi wa kufanya mambo yenye manufaa zaidi.”​—Briana.

 Kanuni ya Biblia: “Kila mmoja na achunguze matendo yake mwenyewe, kisha atakuwa na sababu ya kushangilia kuhusiana na yeye mwenyewe, na si kwa kujilinganisha na mtu mwingine.”​—Wagalatia 6:4.

a Kutoka kwenye kitabu iGen.

b Kutoka kwenye kitabu Why Gender Matters.

c Kutoka kwenye kitabu Glow Kids.