Hamia kwenye habari

VIJANA HUULIZA

Ninaweza Kukabilianaje na Kubalehe?

Ninaweza Kukabilianaje na Kubalehe?

 “Kipindi cha kubalehe ni kigumu sana kwa wasichana. Wanapatwa na maumivu mengi na wanachanganyikiwa sana. Karibu kila jambo linaonekana kuwa baya!”​—Oksana.

 “Ningekuwa na furaha halafu baada ya muda mfupi ningehuzunika. Sijui ikiwa ni kawaida kwa wavulana kuhisi hivyo, lakini hilo lilinipata.”​—Brian.

 Kubalehe kunaweza kulinganishwa na mchezo wa vigari vinavyoteleza kwa kasi juu ya reli iliyopinda-pinda (roller-coaster). Kipindi hicho kinaweza kusisimua na wakati huohuo kuogopesha! Unaweza kukabilianaje na hali hiyo?

 Kubalehe ni nini?

 Kubalehe ni kipindi cha maisha kinachotokeza mabadiliko ya kimwili na kihisia ili kuwa mtu mzima. Katika kipindi hiki, mwili na homoni zinabadilika kwa kasi ili kukuandaa uwe na uwezo wa kuzaa.

 Jambo hilo halimaanishi kwamba unastahili kuwa mzazi. Badala yake, kubalehe ni ishara ya kuachana na utoto na kuwa mtu mzima—jambo linaloweza kufurahisha na wakati uleule kuhuzunisha.

 Swali: Unafikiri kwa kawaida mtu anaweza kuanza kubalehe akiwa na umri gani?

  • 8

  • 9

  • 10

  • 11

  • 12

  • 13

  • 14

  • 15

  • 16

 Jibu: Mtu anaweza kuanza kubalehe akiwa na umri wowote kati ya huo uliotajwa.

 Hivyo, hupaswi kuwa na wasiwasi unapokaribia kuwa na umri wa miaka 15 au 16 na bado hujaanza kubalehe au ikiwa umeanza kubalehe ukiwa na miaka chini ya kumi. Mtu hubalehe kwa wakati wake mwenyewe kwa kutegemea mifumo ya mwili ambayo haiwezi kudhibitiwa.

Kubalehe kunaweza kulinganishwa na mchezo wa vigari vinavyoteleza kwa kasi juu ya reli iliyopinda (roller-coaster). Kipindi hicho kinaweza kusisimua na kuogopesha. Hata hivyo, unaweza kujifunza jinsi ya kukabiliana nacho

 Mabadiliko ya kimwili

 Badiliko linaloonekana zaidi wakati wa kubalehe ni ukuzi wa haraka. Tatizo ni kwamba sehemu za mwili wako hazikui kwa kasi ileile. Kwa hiyo, usishangae ikiwa unafanya mambo fulani kwa njia isiyofaa. Uwe na uhakika kwamba kuna wakati mambo yatakuwa sawa.

 Mabadiliko mengine ya kimwili yanayotokana na kubalehe.

 Wavulana wanapobalehe:

  •   Viungo vya uzazi hukua

  •   Wanaota nywele kwapani, kwenye viungo vya uzazi, na kuota ndevu

  •   Sauti hubadilika

  •   Viungo vya uzazi husisimka bila kutarajia na kutokwa na shahawa usiku

 Wasichana wanapobalehe:

  •   Matiti hukua

  •   Nywele huota kwapani na kwenye viungo vya uzazi

  •   Hedhi huanza

 Wote wanapobalehe:

  •   Mwili hutoa harufu kwa sababu ya mchanganyiko wa jasho na bakteria.

     Pendekezo: Ili kudhibiti harufu unaweza kuoga mara kwa mara na kutumia marashi ya kujipaka kwapani au kuzuia harufu.

  •   Chunusi zinazosababishwa na bakteria kwenye tezi za mafuta hutokea.

     Pendekezo: Ingawa kudhibiti chunusi si rahisi, kuosha uso wako kwa ukawaida na kutumia dawa za kusafisha ngozi kunaweza kusaidia.

 Mabadiliko ya kihisia

 Homoni zinazosababisha mabadiliko ya haraka katika mwili wakati wa kubalehe zinaweza kuathiri hisia zako. Huenda hisia zako zikabadilika-badilika ghafla.

 “Leo unalia, kesho uko sawa. Dakika moja umekasirika, halafu ghafla unajifungia chumbani ukiwa umevunjika moyo.”​—Oksana.

 Vijana wengi pia wanakuwa na wasiwasi sana wanapobalehe, wanahisi wanachunguzwa na kuchambuliwa na kila mtu. Kinachofanya hali iwe mbaya zaidi ni kwamba mwili wako unabadilika haraka sana!

 “Nilipoanza kubalehe, nilianza kutembea kizembe na kuvaa mashati makubwa kimakusudi. Ingawa nilijua sababu iliyofanya mwili wangu uanze kubadilika, niliaibika sana na kuwa na wasiwasi mwingi. Sikujihisi kama mtu wa kawaida.”​—Janice.

 Huenda badiliko kubwa zaidi la kihisia utakalopata, ni mtazamo wako kuelekea watu wa jinsia tofauti.

 “Niliacha kufikiri kwamba wavulana wote walikuwa wasumbufu. Nilianza kuvutia na baadhi yao. Mara nyingi mazungumzo yangu na wasichana wengine yalihusisha ‘nani anampenda nani.’”​—Alexis.

 Baadhi ya vijana wanapoanza kubalehe wanatambua kwamba wanaanza kuvutiwa na watu wa jinsia yao. Ikiwa unapatwa na hali hii, usikate kauli kwamba wewe ni shoga. Katika visa vingi, hisia hizo hupotea baada ya muda.

 “Kwa sababu ya kujilinganisha sana na wavulana wengine, nilianza kuvutiwa nao. Baada ya muda niliacha kuvutiwa na wavulana na nikaanza kuvutiwa zaidi na wasichana. Sasa sina tena hisia za kuvutiwa na wavulana wenzangu.”​—Alan .

 Kile unachoweza kufanya

  •    Jitahidi kuwa na mtazamo unaofaa. Ukweli ni kwamba kubalehe ni badiliko la kimwili na kihisia unalohitaji. Unaweza kupata ujasiri kwa kusoma maneno ya mtunga zaburi Daudi, aliyesema hivi: “Nimeumbwa kwa njia ya ajabu yenye kuogopesha.”​—Zaburi 139:14.

  •   Epuka kujilinganisha na wengine, na kukazia sana fikira sura yako. Biblia inasema hivi: “Mwanadamu huona kile kinachoonekana kwa macho, lakini Yehova huona jinsi moyo ulivyo.”​—1 Samweli 16:7.

  •   Fanya mazoezi na upumzike vya kutosha. Ukilala vya kutosha utaepuka kuudhika haraka, hutakuwa na mkazo mkubwa, na hutashuka moyo sana.

  •   Epuka kujichambua sana. Je, ni kweli kwamba kila mtu anakutazama kwa makini? Hata ikiwa watu watasema mambo fulani kuhusu ukuzi wako, uwe na usawaziko. Biblia inasema hivi: “Usiweke moyoni mwako maneno yote ambayo huenda watu wakasema.”​ —Mhubiri 7:​21.

  •   Jifunze kudhibiti tamaa ya ngono ili usitende kupatana nayo. Biblia inasema hivi: “Ukimbieni uasherati! . . . Yeye aliye na mazoea ya kufanya uasherati anautendea dhambi mwili wake mwenyewe.”​—1 Wakorintho 6:18.

  •   Zungumza na wazazi wako au mtu mzima unayemwamini. Ni kweli kwamba inaweza kuwa vigumu mwanzoni. Lakini msaada utakaopata utakunufaisha sana.​—Methali 17:17.

 Jambo kuu: Kipindi cha kubalehe kina changamoto. Lakini kinakupa nafasi nzuri ya kukua kimwili, kiakili, kihisia, na kiroho.​—1 Samweli 2:26.