Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA ISHIRINI NA TATU

Alijifunza Kusamehe Kutoka kwa Bwana Wake

Alijifunza Kusamehe Kutoka kwa Bwana Wake

1. Ni pindi gani ambayo huenda ilikuwa mbaya zaidi katika maisha ya Petro?

PETRO hangesahau kamwe ile pindi yenye kuhuzunisha Yesu alipomtazama. Je, aliona kwamba Yesu amekasirika? Hatuwezi kusema kwa uhakika; lakini Maandiko yanasema: “Bwana akageuka, akamtazama Petro.” (Luka 22:61) Yesu alipomtazama, Petro aliona uzito wa kosa lake. Alitambua alikuwa amefanya jambo ambalo Yesu alitabiri, ingawa Petro alikuwa amesisitiza kwamba hangeweza kamwe kulifanya—yaani, kumkana Bwana wake mpendwa. Petro alikuwa ameshuka moyo sana, labda hiyo ilikuwa pindi mbaya zaidi katika maisha yake.

2. Petro alihitaji kujifunza somo gani, na tutafaidikaje na mfano wake?

2 Lakini bado kulikuwa na matumaini. Kwa sababu Petro alikuwa na imani yenye nguvu, angepata nafasi ya kurekebisha kosa lake na kujifunza mojawapo ya mambo makuu ambayo Yesu alifundisha. Alijifunza kusamehe. Sote tunahitaji kujifunza somo hilo, acheni tuone jinsi Petro alivyojifunza kusamehe.

Alihitaji Kujifunza Mengi

3, 4. (a) Petro alimuuliza Yesu swali gani na huenda Petro alifikiria nini? (b) Yesu alionyeshaje kwamba Petro alikuwa ameathiriwa na roho iliyokuwa imeenea siku hizo?

3 Miezi sita hivi mapema akiwa kwenye jiji la kwao la Kapernaumu Petro alimuuliza Yesu: “Bwana, ndugu yangu atanitendea dhambi mara ngapi nami nimsamehe? Mpaka mara 7?” Yaelekea Petro alifikiri kwamba ingetosha kusamehe mara saba. Viongozi wa kidini wa siku hizo walifundisha kwamba mtu alipaswa kusamehe mara tatu tu! Yesu akamjibu: “Si, Mpaka mara 7, bali, Mpaka mara 77.”​—Mt. 18:21, 22.

4 Je, Yesu alimaanisha kwamba Petro alipaswa kuweka rekodi ya makosa? Hapana; kwa kumwambia asamehe mara 77 badala ya 7, Yesu alimaanisha hakuna mwisho wa kusamehe. (1 Kor. 13:4, 5) Yesu alionyesha kwamba Petro alikuwa ameathiriwa na roho ngumu ya kutosamehe na ya kuweka hesabu ya makosa iliyokuwa imeenea sana siku hizo. Lakini kama Mungu, tunapaswa kusamehe bila kukoma.​Soma  1 Yohana 1:7-9.

5. Huenda tukakumbuka umuhimu wa kusamehe nyakati gani?

5 Petro hakubishana na Yesu. Lakini, je, Petro alielewa somo alilofunzwa na Yesu? Nyakati nyingine tunaelewa umuhimu wa kusamehe tunapokumbuka jinsi sisi wenyewe tunavyohitaji kusamehewa. Hivyo, acheni tuchunguze mambo yaliyotukia kabla ya kifo cha Yesu. Wakati huo mgumu, Yesu alihitaji kumsamehe Petro makosa mengi.

Alisamehewa Mara Nyingi

6. Petro aliitikiaje Yesu alipojaribu kuwafundisha mitume kuhusu unyenyekevu, lakini Yesu alimtendeaje?

6 Ilikuwa pindi muhimu—usiku wa mwisho kabla ya kifo cha Yesu. Alikuwa na mengi ya kuwafundisha mitume wake—kwa mfano, kuhusu unyenyekevu. Yesu aliweka mfano wa unyenyekevu kwa kuwaosha miguu, kazi iliyofanywa na mfanyakazi wa hali ya chini kabisa. Mwanzoni, Petro alipinga tendo hilo la Yesu. Kisha akakataa kuoshwa miguu. Halafu akasisitiza kwamba Yesu amwoshe si miguu tu bali pia mikono na kichwa! Yesu alionyesha subira na kwa utulivu akaeleza umuhimu na maana ya jambo alilokuwa akifanya.​—Yoh. 13:1-17.

7, 8. (a) Petro alimkoseaje tena Yesu? (b) Yesu aliendeleaje kusamehe na kuonyesha fadhili?

7 Muda mfupi baadaye, Yesu alihitaji kumvumilia tena Petro. Mitume walianza kubishana kuhusu ni nani aliyekuwa mkuu zaidi kati yao, na bila shaka, Petro alishiriki katika mabishano hayo yenye aibu yaliyofunua kiburi chao. Lakini Yesu akawarekebisha kwa fadhili na hata akawapongeza kwa jambo zuri walilofanya, yaani, kuwa waaminifu kwa kushikamana na Bwana wao. Hata hivyo, akatabiri kwamba wote wangemwacha. Lakini Petro akasema angeshikamana na Yesu hadi kifo. Kinyume cha hilo, Yesu alisema Petro angemkana Bwana wake mara tatu kabla ya jogoo kuwika mara mbili usiku huo. Kisha, Petro akapinga maneno ya Yesu na kujivuna kwamba angekuwa mwaminifu zaidi ya mitume wengine wote!​—Mt. 26:31-35; Marko 14:27-31; Luka 22:24-28; Yoh. 13:36-38.

8 Je, Yesu alikuwa amechoka kumvumilia Petro? Katika pindi hiyo ngumu, Yesu aliendelea kutafuta sifa nzuri za wanafunzi wake wasio wakamilifu. Ingawa Yesu alijua Petro angemkana, alisema: “Nimeomba dua kwa ajili yako ili imani yako isififie; na wewe, mara tu utakapokuwa umerudi, watie nguvu ndugu zako.” (Luka 22:32) Hivyo, akaonyesha alikuwa na hakika Petro angetubu makosa yake na kuendelea na utumishi kwa uaminifu. Yesu alikuwa mwenye kusamehe na mwenye fadhili kama nini!

9, 10. (a) Kwa nini Petro alihitaji kurekebishwa katika bustani ya Gethsemane? (b) Makosa ya Petro yanatukumbusha nini?

9 Baadaye, katika bustani ya Gethsemane, Petro alihitaji kurekebishwa tena na tena. Yesu aliwaambia Petro, Yakobo, na Yohana, waendelee kukesha alipokuwa akisali. Yesu alikuwa na maumivu makali ya kihisia na alihitaji msaada, lakini Petro na wenzake waliendelea kulala. Yesu alisema maneno haya yanayoonyesha huruma na msamaha: “Bila shaka, roho inataka, lakini mwili ni dhaifu.”​—Marko 14:32-41.

10 Punde si punde, umati wa watu waliobeba mienge, mapanga, na marungu ukafika. Huo ulikuwa wakati wa kutenda kwa tahadhari na busara. Lakini, kwa ghafula Petro akachomoa upanga wake na kumshambulia Malko, mtumwa wa kuhani mkuu, na kulikata sikio lake. Kwa utulivu Yesu alimkosoa Petro, akamponya Malko, kisha akataja kanuni ya kuepuka kutenda kwa jeuri ambayo inafuatwa na wafuasi wake mpaka leo. (Mt. 26:47-55; Luka 22:47-51; Yoh. 18:10, 11) Tayari Yesu alikuwa amemsamehe Petro mara nyingi. Makosa yake yanatukumbusha kwamba “sisi sote hujikwaa mara nyingi.” (Soma Yakobo 3:2.) Kila mmoja wetu anahitaji kusamehewa na Mungu kila siku. Lakini kuna mengi yaliyomsubiri Petro usiku huo. Bado angefanya makosa mengine.

Petro Afanya Kosa Kubwa Zaidi

11, 12. (a) Petro alionyeshaje ujasiri kwa kiasi fulani baada ya Yesu kukamatwa? (b) Petro alishindwaje kufanya jambo alilodai kwamba angefanya?

11 Yesu aliuambia umati uliokuja kumkamata kwamba ikiwa walikuwa wanamtafuta yeye, walipaswa kuwaacha mitume wake waende. Petro alitazama asijue la kufanya umati huo ulipomkamata na kumfunga Yesu. Kisha, Petro pamoja na mitume wenzake wakakimbia.

12 Petro na Yohana waliacha kukimbia labda walipokaribia nyumba ya Anasi ambaye hapo awali alikuwa Kuhani Mkuu, na Yesu alipelekwa huko kwanza ili kuhojiwa. Yesu alipotolewa hapo, Petro na Yohana walimfuata lakini ‘wakiwa mbali kiasi.’ (Mt. 26:58; Yoh. 18:12, 13) Petro hakuwa mwoga. Alionyesha ujasiri kwa kumfuata Yesu. Umati huo ulikuwa na silaha, na tayari Petro alikuwa amemjeruhi moja wao. Hata hivyo, katika tukio hili Petro haonyeshi upendo mshikamanifu ambao alidai alikuwa nao, yaani, kuwa tayari kufa pamoja na Bwana wake ikihitajika.​—Marko 14:31.

13. Ni njia gani pekee inayofaa ya kumfuata Kristo?

13 Kama Petro, wengi leo wangependa kumfuata Kristo ‘wakiwa mbali kiasi,’ ili watu wengine wasitambue. Lakini kama Petro mwenyewe alivyoandika baadaye, njia pekee ya kumfuata Kristo inavyofaa ni kukaa karibu zaidi naye kadiri iwezekanavyo, kuiga kielelezo Chake katika mambo yote, hata iweje.​—Soma 1 Petro 2:21.

14. Petro alikaa wapi usiku kesi ya Yesu ilipokuwa ikiendelea?

14 Petro aliufuata umati kwa tahadhari hadi kwenye lango la nyumba moja ya kifahari huko Yerusalemu. Ilikuwa nyumba ya Kayafa, kuhani mkuu tajiri na mwenye mamlaka. Kwa kawaida nyumba kama hizo zilizungukwa na ua na zilikuwa na lango upande wa mbele. Petro alipofika langoni, alikatazwa kuingia ndani. Tayari Yohana alikuwa ameingia kwa sababu alimjua kuhani mkuu, hivyo, akamwomba mlinda lango amruhusu Petro aingie. Inaonekana Petro hakukaa karibu na Yohana; wala hakuingia ndani ya nyumba ili awe karibu na Bwana wake. Alikaa uani ambako watumwa na watumishi walikuwa wakiota moto usiku, huku wakiwatazama mashahidi wa uwongo wakiingia na kutoka ndani ya nyumba ili kutoa ushahidi dhidi ya Yesu.​—Marko 14:54-57; Yoh. 18:15, 16, 18.

15, 16. Eleza jinsi utabiri wa Yesu kuhusu kukanwa mara tatu ulivyotimia.

15 Kwa sababu ya mwangaza wa moto, sasa msichana aliyemruhusu Petro aingie alimtambua. Akamshutumu hivi: “Wewe, pia, ulikuwa pamoja na Yesu Mgalilaya!” Petro alishtuka, akasema hamjui Yesu na kwamba hakuelewa kile ambacho msichana huyo alisema. Alienda kusimama karibu na lango ili asionekane, lakini msichana mwingine akamtambua na kusema jambo lilelile: “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.” Lakini Petro akaapa: “Simjui mtu huyo!” (Mt. 26:69-72; Marko 14:66-68) Labda baada ya kumkana Yesu mara ya pili, Petro alisikia jogoo akiwika, lakini alikuwa amevurugika kiasi cha kwamba hakukumbuka unabii ambao Yesu alikuwa ametoa saa chache mapema.

16 Muda mfupi baadaye, bado Petro alikuwa anajaribu kujificha. Lakini watu fulani waliokuwa wamesimama uani wakamkaribia. Mmoja wao alikuwa mtu wa ukoo wa Malko, yule mtumwa ambaye Petro alimkata sikio. Akamwambia Petro: “Mimi nilikuona katika bustani pamoja naye, sivyo?” Petro akaona kwamba anapaswa kuwathibitishia kuwa wamekosea. Hivyo, akaapa kuhusu jambo hilo, inaelekea alisema ikiwa alikuwa akisema uwongo alipaswa kulaaniwa. Sasa alikuwa amekana mara ya tatu. Punde tu aliposema maneno hayo, jogoo akawika, na ilikuwa mara ya pili kwa Petro kusikia jogoo akiwika usiku huo.​—Yoh. 18:26, 27; Marko 14:71, 72.

“Bwana akageuka, akamtazama Petro”

17, 18. (a) Petro alitendaje alipotambua kwamba alikuwa amemkosea sana Bwana wake? (b) Huenda Petro alifikiria nini?

17 Yesu alikuwa ametoka nje na kusimama roshani. Wakati huo, kama ilivyotajwa mwanzoni mwa sura hii, macho ya Yesu na Petro yalikutana. Ndipo Petro akatambua jinsi alivyokuwa amemkosea Bwana wake. Petro aliondoka uani akijihisi mwenye hatia sana. Alienda kwenye barabara za jiji zilizoangazwa kwa mwezi uliokuwa ukitua. Machozi yalimlengalenga. Hakuwa anaona vizuri. Kisha akaanza kulia kwa uchungu.​—Marko 14:72; Luka 22:61, 62.

18 Mtu anapotambua uzito wa kosa kama hilo, ni rahisi sana kufikiri kwamba dhambi yake ni nzito mno isiweze kusamehewa. Huenda hata Petro alifikiri hivyo. Je, Petro angesamehewa?

Je, Petro Angesamehewa?

19. Petro alihisije kuhusu makosa yake, na ingawa hivyo tunajuaje kwamba hakukata tamaa?

19 Petro alikuwa na uchungu mwingi sana asubuhi ilipofika, na matukio ya siku hiyo yalizidisha tu uchungu wake. Lazima alijuta Yesu alipokufa siku hiyo alasiri baada ya kuteswa kwa saa nyingi! Haikosi Petro aliumia sana kila alipofikiria jinsi alivyochangia uchungu wa Bwana wake katika siku Yake ya mwisho duniani akiwa mwanadamu. Ingawa Petro alikuwa na huzuni nyingi, hakukata tamaa. Tunajua hivyo kwa sababu muda mfupi baadaye Petro alianza tena kushirikiana na ndugu zake. (Luka 24:33) Bila shaka, mitume wote walijuta kwa sababu ya vitendo vyao usiku huo mgumu, na walitiana moyo kwa kadiri fulani.

20. Tunaweza kujifunza nini kutokana na jinsi Petro alivyopambana na huzuni?

20 Hivyo, tunaona jinsi Petro alivyofanya uamuzi bora. Mtumishi wa Mungu anapofanya kosa, jambo muhimu si uzito wa kosa lake, bali ni jitihada anazofanya ili kuinuka tena na kurekebisha mambo. (Soma Methali 24:16.) Petro alionyesha imani ya kweli kwa kukusanyika na ndugu zake licha ya kushuka moyo. Mtu anapolemewa na huzuni au majuto, anaweza kushawishiwa kujitenga, lakini hilo ni hatari. (Met. 18:1) Jambo la hekima ni kukaa karibu na waamini wenzake ili awe tena na nguvu kiroho.​—Ebr. 10:24, 25.

21. Kwa vile alikusanyika na ndugu zake wa kiroho, Petro alisikia habari gani?

21 Akiwa pamoja na ndugu zake wa kiroho, Petro alisikia habari zenye kushtua kwamba mwili wa Yesu haukuwa kaburini. Petro na Yohana walikimbia kwenda kwenye kaburi lililozibwa ambamo Yesu alikuwa amezikwa. Yohana, ambaye inaelekea alikuwa kijana, alifika kwanza. Lakini akasita kuingia alipokuta kaburi likiwa wazi. Petro hakusita. Ingawa alikuwa akihema, aliingia ndani ya kaburi. Kwa kweli, lilikuwa tupu!​—Yoh. 20:3-9.

22. Nini kilichomfanya Petro asiwe na shaka na aache kuhuzunika?

22 Je, Petro aliamini kwamba Yesu alikuwa amefufuliwa? Mwanzoni hakuamini, ingawa wanawake waaminifu walisema kwamba malaika waliwatokea na kuwaambia Yesu alikuwa amefufuka. (Luka 23:55–24:11) Kufikia jioni, Petro hakuwa tena na shaka wala huzuni. Yesu alikuwa hai akiwa kiumbe wa roho mwenye nguvu! Aliwatokea mitume wake wote. Lakini kwanza alifanya jambo fulani la faragha. Mitume walisema hivi siku hiyo: “Kwa kweli Bwana alifufuliwa naye alimtokea Simoni!” (Luka 24:34) Pia, baadaye mtume Paulo aliandika kuhusu siku hiyo ya pekee ambapo Yesu “alimtokea Kefa, kisha wale kumi na wawili.” (1 Kor. 15:5) Kefa na Simoni ni majina mengine ya Petro. Yesu alimtokea Petro siku hiyo—inaelekea akiwa peke yake.

Yesu alihitaji kumsamehe Petro makosa mengi, na je, si ni kweli kwamba sisi pia tunahitaji kusamehewa kila siku?

23. Kwa nini Wakristo wanaotenda dhambi nzito wanahitaji kukumbuka mfano wa Petro?

23 Biblia haisemi kilichotendeka Yesu alipokutana na Petro. Ni Yesu na Petro tu wanaojua. Tunaweza kuwazia jinsi Petro alivyofurahi kumwona Bwana wake mpendwa akiwa hai tena, na kupata nafasi ya kuonyesha huzuni na toba yake. Zaidi ya yote, Petro alitamani kusamehewa. Tuna hakika kwamba Yesu alimsamehe kabisa. Leo, Wakristo wanaotenda dhambi nzito wanahitaji kukumbuka kisa cha Petro. Hatupaswi kamwe kufikiri Mungu hawezi kutusamehe. Yesu alionyesha wazi kwamba Baba yake ‘husamehe kwa njia kubwa.’​—Isa. 55:7.

Uthibitisho Zaidi wa Msamaha

24, 25. (a) Eleza ilivyokuwa usiku ambao Petro alienda kuvua samaki kwenye Bahari ya Galilaya. (b) Petro alitendaje Yesu alipofanya muujiza asubuhi iliyofuata?

24 Yesu aliwaambia mitume wake waende Galilaya, ambako wangekutana naye tena. Walipofika huko, Petro aliamua kwenda kuvua samaki katika Bahari ya Galilaya. Mitume kadhaa walimfuata. Kwa mara nyingine tena, Petro alijikuta amerudia maisha yake ya zamani. Bila shaka, alikumbuka mengi kutokana na mlio wa mbao za mashua, sauti za mawimbi, na nyavu za kuvua samaki. Hata hivyo, wanaume hao hawakuvua samaki hata mmoja usiku wote.​—Mt. 26:32; Yoh. 21:1-3.

Petro akatoka kwenye mashua na kuogelea mpaka ufuoni

25 Lakini, kulipopambazuka, mtu fulani aliwaita akiwa ufuoni na kuwahimiza watupe nyavu zao upande ule mwingine wa mashua. Walitii na kuvua samaki 153! Petro alimtambua mtu huyo. Akatoka kwenye mashua na kuogolea mpaka ufuoni. Wakiwa ufuoni, Yesu aliwapa chakula cha samaki aliyepikwa kwenye moto wa makaa. Kisha, Yesu akamkazia fikira Petro.—Yoh. 21:4-14.

26, 27. (a) Yesu alimpa Petro nafasi ya kufanya nini mara tatu? (b) Yesu alithibitishaje kwamba alikuwa amemsamehe kabisa Petro?

26 Yesu alimuuliza Petro kama alimpenda Bwana wake “kuliko hawa”—inaonekana akielekezea kidole samaki wengi waliokuwa wamevuliwa. Je, Petro alipenda biashara ya uvuvi kuliko Yesu? Kama vile Petro alivyomkana Bwana wake mara tatu, sasa Yesu alimpa nafasi ya kuthibitisha upendo wake mara tatu mbele ya mitume wenzake. Alipokuwa akifanya hivyo, Yesu alimweleza jinsi ya kuonyesha upendo huo: kwa kutanguliza utumishi mtakatifu, kulisha, kuimarisha, na kuchunga kondoo wa Kristo, yaani, wafuasi Wake waaminifu.​—Luka 22:32; Yoh. 21:15-17.

27 Hivyo, Yesu akathibitisha kwamba yeye na Baba yake wangeendelea kumtumia Petro. Mtume huyo angetimiza daraka muhimu katika kutaniko chini ya mwongozo wa Kristo. Huo ni uthibitisho ulioje kwamba Yesu alikuwa amemsamehe Petro kabisa! Kwa kweli, Petro alithamini rehema alizoonyeshwa na hilo lilimgusa moyo.

28. Petro alikujaje kuishi kupatana na jina lake?

28 Petro aliendelea kutimiza daraka lake kwa miaka mingi. Aliwaimarisha ndugu zake, kama vile Yesu alivyomwamuru usiku uliotangulia kifo Chake. Kwa subira na fadhili, Petro aliwachunga na kuwalisha wafuasi wa Kristo. Simoni aliishi kupatana na jina alilopewa na Yesu—Petro, au Mwamba—kwa kuwa imara, mwenye nguvu, na mwenye kutegemeka kutanikoni. Hilo linaonekana katika barua zake mbili zenye upendo ambazo zilikuja kuwa vitabu muhimu vya Biblia. Barua hizo pia zinaonyesha kwamba Petro hakuwa amesahau jambo alilojifunza kutoka kwa Yesu kuhusu kusamehe.​—Soma 1 Petro 3:8, 9; 4:8.

29. Tunawezaje kuiga imani ya Petro na rehema ya Bwana wake?

29 Ni vizuri pia tujifunze somo hilo. Je, sisi humwomba Mungu kila siku atusamehe makosa yetu mengi? Je, tunakubali msamaha wa Mungu na kuamini kwamba unatufanya tuwe safi? Na je, tunawasamehe wengine? Tukifanya hivyo, tutaiga imani ya Petro—na rehema ya Bwana wake.