Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 MAHOJIANO | WENLONG HE

Mwanafizikia Aeleza kwa Nini Anamwamini Mungu

Mwanafizikia Aeleza kwa Nini Anamwamini Mungu

WENLONG HE alianza kusomea fizikia huko Suzhou, Jimbo la Jiangsu, China. Yeye husaidia kuhariri jarida fulani la kimataifa linalohusu teknolojia na ameandika habari nyingi za kisayansi. Kwa sasa, Wenlong He anafanya kazi katika Chuo Kikuu cha Strathclyde, Scotland. Alipokuwa kijana aliamini mageuzi, lakini baadaye alifikia mkataa kwamba uhai uliumbwa. Mwandishi wa Amkeni! alimhoji kuhusu imani yake.

Tueleze kuhusu malezi yako.

Nilizaliwa mwaka wa 1963 na nililelewa China, katika kijiji kilicho kusini mwa Mto Yangtze, Jimbo la Jiangsu. Ni eneo lenye joto na mvua linalozalisha chakula kwa wingi, na linajulikana kama nchi ya mchele na samaki. Nikiwa mtoto nilijiuliza: ‘Kwa nini kuna vyakula vingi vitamu duniani? Je, vilijitokeza vyenyewe? Ni nini kilichokuja kwanza—kuku au yai?’ Watu wengi nchini China hawaamini kuna Mungu, na hivyo, tulifundishwa mageuzi shuleni.

Namna gani familia yako?

Wazazi wangu hawakuamini kuna Mungu. Mama yangu alikuwa mkulima, naye baba alikuwa mchora-ramani za ujenzi na alianzisha kampuni ya ujenzi. Mimi ndiye mtoto wao wa kwanza kati ya wana watano. Kwa kusikitisha, ndugu zangu wawili walikufa wakiwa wachanga. Hilo lilinihuzunisha sana na nilijiuliza: ‘Kwa nini watu hufa? Je, nitawaona wadogo zangu tena?’

Kwa nini ulichagua somo la sayansi?

Nilitaka kusomea fizikia kwa sababu nilivutiwa na ulimwengu wa asili na nilifikiri fizikia ingejibu maswali ambayo nilijiuliza tangu utotoni.

Unafanya utafiti kuhusu nini?

Ninachunguza njia za kuongeza mwendo wa atomu zenye umeme hadi kufikia kasi ya nuru. Ninafanya hivyo ili kuchunguza muundo wa atomu. Ninachunguza pia jinsi ya kutokeza mnururisho  wenye nguvu zilizo kati ya mnururisho wa nguvu-sumaku (microwave) na mnururisho wa miale isiyoonekana (infrared). Ingawa utafiti wangu unakusudiwa kutumiwa katika biashara, unahusiana pia na jitihada za kuelewa jinsi ulimwengu ulivyotokea.

Ni nini kilichofanya upendezwe na Biblia?

Mwaka wa 1998, Mashahidi wawili wa Yehova walinitembelea nyumbani. Walijitolea kujibu maswali yangu kwa kutumia Biblia. Mke wangu, Huabi, ambaye pia ni mwanasayansi, alijiunga nasi. Ilikuwa mara ya kwanza kwetu kuona Biblia, lakini tulivutiwa na ushauri wa Biblia wenye busara. Tuliona jinsi wenzi wa ndoa Mashahidi waliotutembelea walivyonufaika kwa kufuata kanuni za Biblia. Walikuwa na furaha na waliishi maisha yasiyo na mambo mengi. Hata hivyo, yale ambayo Biblia inasema kumhusu Mungu yalifanya nijiulize tena ikiwa ulimwengu uliumbwa. Nikiwa mwanafizikia, kazi yangu ni kuelewa ulimwengu unaotuzunguka. Hivyo, niliamua kuchunguza kwa makini uthibitisho wa kisayansi.

Nikiwa mwanafizikia, kazi yangu ni kuelewa ulimwengu unaotuzunguka. Hivyo, niliamua kuchunguza kwa makini utafiti wa kisayansi

Ulichunguza mambo gani?

Kwanza, nilijua kwamba mfumo wowote hauwezi kuwa na utaratibu au kuwa na mpangilio bila msaada wa nguvu fulani. Hiyo ni sheria ya pili ya fizikia inayohusiana na nishati (thermodynamics). Nilifikia mkataa kwamba lazima vilibuniwa na Muumba kwa vile kuna utaratibu wa hali ya juu katika ulimwengu na viumbe vilivyo duniani. Jambo la pili nililochunguza linahusiana na jinsi ulimwengu ulivyobuniwa hasa ili kutegemeza uhai.

Ulipata uthibitisho gani?

Uhai wote duniani hutegemea nishati ya jua. Nishati hiyo husafiri angani ikiwa mnururisho. Inafika duniani ikiwa katika aina mbalimbali za mawimbi. Miale hatari ya gama ndiyo mifupi zaidi. Kisha miale ya eksirei, urujuanimno, nuru inayoonekana, infrared, sumaku-umeme, na mawimbi marefu zaidi ni ya redio. Kwa kustaajabisha, angahewa letu huzuia mnururisho hatari na kuruhusu mnururisho unaohitajika kufika duniani.

Kwa nini ulipendezwa na jambo hilo?

Nilivutiwa na simulizi la Biblia kuhusu uumbaji na jinsi linavyosema kuhusu nuru. Linasema: “Mungu akasema: ‘Kuwe na nuru.’ Kukawa na nuru.” * Nuru inayoonekana ni karibu nusu tu ya mawimbi ya mnururisho wa jua, hata hivyo nuru ni muhimu kwa uhai. Mimea huhitaji nuru ili kutengeneza chakula chetu, nasi tunahitaji nuru ili kuona. Uwezo wa angahewa wa kuruhusu nuru kufika duniani haukujitokeza wenyewe. La kustaajabisha zaidi ni kiwango kidogo cha mnururisho wa urujuanimno unaofika duniani.

Kwa nini hilo ni jambo muhimu?

Tunahitaji kiasi kidogo cha urujuanimno. Tunahitaji kiasi kidogo cha mnururisho huo kwenye ngozi yetu ili kutengeneza vitamini D, ambayo ni muhimu ili kuimarisha mifupa na kuzuia kansa na magonjwa mengine. Hata hivyo, kiwango kikubwa cha mnururisho huo husababisha kansa ya ngozi na ugonjwa fulani wa macho. Kiasili, angahewa huruhusu kiwango kidogo tu cha urujuanimno kufika duniani—kiwango kinachofaa kabisa. Ninaamini hilo linathibitisha kwamba kuna Muumba aliyebuni dunia kwa ustadi ili itegemeze uhai.

Hatua kwa hatua, mimi na Huabi tulisadiki kwamba kuna Muumba, ambaye alitumia roho yake kuwaongoza wale walioandika Biblia. Mwaka wa 2005, tulibatizwa na kuwa Mashahidi wa Yehova, na sasa tunawafundisha wengine Biblia.