Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

MAHOJIANO | DAKT. GENE HWANG

Mtaalamu wa Hesabu Anaeleza kwa Nini Anamwamini Mungu

Mtaalamu wa Hesabu Anaeleza kwa Nini Anamwamini Mungu

Dakt. Gene Hwang, alizaliwa mwaka 1950 jijini Tainan, nchini Taiwan, na ni profesa wa hesabu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Chung Cheng nchini Taiwan. Pia, ni profesa mstaafu anayeheshimika katika Chuo Kikuu cha Cornell, nchini Marekani, ambapo alifundisha na kufanya utafiti wa takwimu na hesabu za uwezekano. Kwa miaka mingi amekuwa kati ya wataalamu wanaoheshimika katika taaluma ya takwimu, kazi ambayo bado anajihusisha nayo. Alipokuwa kijana, aliamini kwamba uhai ulitokana na mageuzi. Lakini baadaye alibadili maoni yake. Mwandishi wa Amkeni! alimhoji kuhusu kazi yake na imani yake.

Ulijifunza masomo gani ulipokuwa kijana?

Shuleni nilijifunza nadharia ya mageuzi, lakini hakuna aliyeeleza kwa usahihi uhai ulianzaje. Wazazi wangu walipoanza kushirikiana na dini ya Watao, nilizoea kuwasikiliza viongozi wao wa kidini na kuwauliza maswali mengi. Lakini majibu mengi waliyonipa hayakuniridhisha.

Kwa nini uliamua kuwa mtaalamu wa hesabu?

Nilipokuwa shule ya msingi, nilipenda sana somo la hesabu. Hata nilipoenda chuo kikuu bado niliendelea kufurahia masomo ya hesabu. Mimi huvutiwa sana na hesabu iliyochanganuliwa kwa ufupi, na huiona kama sanaa.

Ni nini kilifanya uvutiwe na Biblia?

Mnamo 1978 mke wangu, Jinghuei, alianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, na mara kadhaa nilishiriki mazungumzo hayo. Wakati huo tulikuwa tukiishi Marekani. Jinghuei alikuwa amepata tu shahada ya udaktari wa fizikia, nami nilikuwa nikisomea takwimu katika Chuo Kikuu cha Purdue huko Indiana.

Ulikuwa na maoni gani kuhusu Biblia?

Nilivutiwa na simulizi la Biblia kuhusu jinsi dunia ilivyotayarishwa kwa ajili ya wanadamu. Vipindi sita vya uumbaji vinavyosimuliwa kwa lugha rahisi katika kitabu cha Mwanzo, vinapatana na mambo hakika—tofauti kabisa na hekaya. * Hata hivyo, kwa miaka mingi sikuamini kwamba kuna Muumba.

Kwa nini ilikuwa vigumu kwako kuamini kuna Muumba?

Kuamini kuna Muumba kulimaanisha kwamba ninaikataa dini yangu ya utotoni

Hisia zangu zilihusika. Kuamini kuna Muumba kulimaanisha kwamba ninaikataa dini yangu ya utotoni, kwa sababu Watao hawaamini kwamba kuna Mungu wala Muumba.

Kwa nini maoni yako yalibadilika baadaye?

Kadiri nilivyotafakari jinsi uhai ulivyoanza, ndivyo nilivyosadiki kabisa kwamba lazima kiumbe wa kwanza alikuwa wa ajabu sana. Kwa mfano, alipaswa kuwa na uwezo wa kuzaa, hivyo alihitaji kuwa na habari zilizo katika chembe za urithi na mifumo inayoweza kunakili habari hizo kwa usahihi. Hata chembe ndogo zaidi zinahitaji molekuli ili kufanyiza sehemu zote za chembe mpya na pia kuhifadhi na kuelekeza nishati. Mifumo hiyo ya ajabu inawezaje kujikusanya yenyewe kutoka kwenye kitu kisicho hai? Nikiwa mwanahisabati nisingeweza kukubaliana na wazo hilo. Linazusha maswali mengi sana.

Ni nini kilichokuchochea uchunguze mafundisho ya Mashahidi wa Yehova?

Nilikuwa nimejifunza na Mashahidi wa Yehova mara kadhaa. Lakini, mnamo 1995, nilitembelea Taiwan. Nikiwa huko nikawa mgonjwa na nikahitaji msaada. Ingawa mke wangu alikuwa Marekani, aliwasiliana na Mashahidi wa Yehova nchini Taiwan. Walinikuta nikiwa hoi nje ya hospitali ambayo haikuwa na vitanda vya kutosha. Shahidi mmoja alinichukua na kunipeleka hotelini ili nipumzike. Aliendelea kunitunza kisha akanipeleka kwenye kituo cha afya kwa ajili ya matibabu.

Niliguswa moyo sana na jinsi walivyonijali, na nikakumbuka pindi nyingine ambazo Mashahidi wa Yehova waliitendea familia yangu kwa fadhili. Imani ya Mashahidi wa Yehova imewafanya wawe tofauti. Hivyo nikaanza tena kujifunza nao Biblia. Mwaka uliofuata nikabatizwa.

Je, imani yako inapingana na masomo yako?

Hapana! Katika miaka ya karibuni nilitumia taaluma yangu ya hesabu kuwasaidia wanasayansi waliokuwa wakichunguza jinsi chembe za urithi zinavyofanya kazi. Kujifunza kuhusu chembe za urithi hunisaidia kuuelewa uhai zaidi—jambo ambalo hunifanya nistaajabishwe na hekima ya Muumba.

Toa mfano wa hekima hiyo.

Fikiria jinsi kiumbe kipya kinavyotokezwa. Baadhi ya viumbe kama vile amiba, havina jinsia ya kiume au ya kike. Vijidudu hivyo vilivyo na chembe moja hufanyiza nakala ya habari zao za chembe za urithi na kujigawa sehemu mbili. Hata hivyo, wanyama wengi na mimea huzaliana kwa kuunganisha habari zilizo katika chembe za urithi za wazazi wa kiume na kike. Kwa nini mfumo wa uzazi unaohusisha jinsia mbili ni wa pekee sana?

Utendaji mzima unaohusika katika kuunganisha nusu ya habari zilizo katika chembe za urithi za kiume na za kike ni tata sana hivi kwamba wanamageuzi wanakabili changamoto kubwa kuthibitisha nadharia yao. Ikiwa kwa muda mrefu sana kiumbe kimoja kimekuwa kikijigawanya katika sehemu mbili ili kutokeza kingine, ni lini ambapo mfumo wa uzazi ulijibadili hivi kwamba lazima viumbe viwili viungane ili kutokeza kimoja? Kwa maoni yangu, mfumo wa uzazi unaotegemea jinsia mbili unathibitisha wazi kwamba akili ya Mungu imetumika.

^ fu. 11 Ili kupata habari zaidi kuhusu vipindi vya uumbaji, ona broshua Uhai—Ulitokana na Muumba? iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Inapatikana kwenye Intaneti katika www.pr418.com/sw.