Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa Mimea wa Kufanya Makadirio

Uwezo wa Mimea wa Kufanya Makadirio

MIMEA hutengeneza chakula chake kwa kutumia mwangaza unaotoka kwa jua kupitia mfumo tata unaoitwa usanidi-mwanga (photosynthesis). Mimea fulani iliyochunguzwa ilifunua uwezo mwingine wa pekee wa mimea—inakadiria mwendo ambao itafyonza chakula kwa usiku mzima.

Fikiria hili: Mimea hubadili kaboni-dioksidi kutengeneza wanga na sukari wakati wa mchana. Wakati wa usiku, mimea mingi hutumia hifadhi ya chakula hicho kilichotengenezwa mchana, hivyo inaendelea kupata mahitaji yake na kukua vizuri. Isitoshe, mimea hiyo hutumia chakula hicho kwa mwendo unaofaa kabisa—si haraka sana na si polepole sana—hivi kwamba asubuhi inapofika inakuwa imetumia asilimia 95 hivi ya chakula hicho na inaanza kutengeneza kingine.

Uwezo huo wa mimea wa kukadiria mwendo wa kufyonza chakula uligunduliwa wakati ambapo mmea wa jamii ya haradali unaoitwa Arabidopsis thaliana ulichunguzwa. Watafiti waligundua kwamba mmea huo unagawa chakula kilichohifadhiwa kwa kuzingatia urefu wa usiku, iwe usiku una urefu wa saa 8, 12, au 16. Inaonekana kwamba mimea hiyo hugawa wanga kulingana na muda uliopo kati ya usiku na alfajiri, na hivyo kukadiria mwendo ambao itatumia kufyonza chakula hicho.

Mimea inatambuaje kiasi cha wanga kilichohifadhiwa? Inapimaje wakati? Na inakadiriaje mwendo wa kufyonza chakula? Huenda majibu yatapatikana baada ya utafiti zaidi.

Una maoni gani? Je, uwezo wa mimea wa kufanya makadirio ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?