Hamia kwenye habari

Je, Mashahidi wa Yehova Wanapinga Kupewa Chanjo?

Je, Mashahidi wa Yehova Wanapinga Kupewa Chanjo?

 Hapana. Mashahidi wa Yehova hawapingi chanjo. Tunaona chanjo kuwa jambo ambalo mtu binafsi anapaswa kujiamulia ikiwa inamfaa. Mashahidi wa Yehova wengi wanachagua kupewa chanjo.

 Tunatafuta huduma bora zaidi za afya zinazoweza kupatikana, na pia tunafurahi kuona maendeleo mengi yanayofanyika katika sayansi ya kitiba ili kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa mabaya. Tunathamini jitihada za watu walio na ujuzi wa mambo hayo, na jinsi wanavyotumia ujuzi huo hasa wakati wa majanga.

 Mashahidi wa Yehova wanatoa ushirikiano wanaposhughulika na watu wa serikali wa sekta ya afya. Kwa mfano, tangu ugonjwa wa corona uanze, Mashahidi wa Yehova wameendelea kuweka vikumbusho katika mamia ya lugha katika tovuti hii, inayotia watu moyo watii miongozo iliyowekwa katika eneo wanaloishi. Hili linatia ndani umuhimu wa kukaa umbali unaofaa na wa kufuata sheria zinazohusiana na jinsi watu wanavyojumuika, jinsi ya kutenga wagonjwa, kunawa mikono, na umuhimu wa kuvaa barakoa pamoja na tahadhari nyingine zilizowekwa na wenye mamlaka.—Waroma 13:1, 2.

 Kwa miaka mingi, machapisho ya Mashahidi wa Yehova yamekazia kanuni zifuatazo:

  •   Maamuzi yoyote kuhusu tiba ni ya mtu binafsi.—Wagalatia 6:5.

     “[Gazeti hili] halipendekezi tiba yoyote hususa au dawa ya aina yoyote, na pia halitoi ushauri wowote wa kitiba. Lengo la gazeti hili ni kuandika mambo yaliyofanyiwa utafiti na kuwaachia wasomaji nafasi ya kufanya maamuzi yao wenyewe.”—Amkeni!, Februari 8, 1987 (Kiingereza).

     “Jibu la swali la kwamba wewe au mtoto wako apewe chanjo ni suala la kibinafsi.”—Amkeni!, Agosti 22, 1965 (Kiingereza).

  •   Tunatafuta tiba ya kiafya kwa sababu tunachukulia suala lolote kuhusiana na uhai kwa uzito.—Matendo 17:28.

     “Mashahidi hutumia uwezo wao mbalimbali wa kitiba kusaidia wale wenye matatizo ya afya. Wanapenda uhai na wanataka kufanya kila kitu wanachoweza kufanya kupatana na Maandiko.”—Mnara wa Mlinzi, Julai 1, 1975 (Kiingereza).

     “Mashahidi wa Yehova hukubali dawa na matibabu bila shida. Wanataka kuwa na afya nzuri na maisha marefu. Kwa kweli, kama Mkristo wa karne ya kwanza, Luka, baadhi ya Mashahidi wa Yehova ni madaktari. . . . Mashahidi wa Yehova wanathamini sana bidii na kujitoa kwa wale wanaotoa huduma za afya. Na pia, wanafurahia sana wataalamu hao wanapowasaidia kupata nafuu kutokana na magonjwa yao.”—Mnara wa Mlinzi, Februari 1, 2011.