Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Uraia wa Roma ulikuwa na faida gani kwa mtume Paulo?

Paulo alisema: “Ninakata rufani kwa Kaisari!”

Raia yeyote wa Roma alistahili kupata haki na manufaa fulani alipokuwa mahali popote katika milki hiyo. Alikuwa chini ya sheria ya Roma, na si chini ya sheria za majiji ya mikoa hiyo. Ikiwa angeshtakiwa, angeweza kuchagua ikiwa kesi yake ingesikilizwa kulingana na sheria za eneo hilo, na wakati huo huo alikuwa na haki ya kusikilizwa na mahakama ya Roma. Ikiwa angefanya kosa lililostahili hukumu ya kifo alikuwa na haki ya kukata rufaa kwa maliki.

Basi kwa misingi hiyo, kiongozi mmoja wa Roma wa karne ya kwanza K.W.K. anayeitwa Cicero, alisema hivi: “Ni kosa kisheria kumfunga raia wa Roma; kumpiga mijeledi ni ukatili; kumuua raia wa Roma ni kama kumuua mzazi wako au mtu wa ukoo.”

Mtume Paulo alihubiri katika maeneo mengi ya Milki ya Roma. Biblia inataja visa vitatu ambapo alitumia haki zake akiwa raia wa Roma: (1) Aliwaeleza mahakimu Wafilipi kuwa walikuwa wamekiuka haki zake kwa kumpiga. (2) Alitaja uraia wake wa Roma ili kuepuka kupigwa mijeledi alipokuwa Yerusalemu. (3) Alikata rufaa kwa Kaisari, maliki wa Roma, ili asikilize kesi yake.—Matendo 16:37-39; 22:25-28; 25:10-12.

Wachungaji walilipwa namna gani katika nyakati za Biblia?

Mkataba wa maandishi ya kikabari wa mauzo ya kondoo na mbuzi, wa mwaka wa 2050 K.W.K. hivi

Yakobo, baba wa ukoo alichunga mifugo ya Labani mjomba wake kwa miaka 20. Kwa miaka 14 ya kwanza alipewa binti wawili wa Labani, na kwa miaka 6 iliyobaki alipewa mifugo ikiwa malipo. (Mwanzo 30:25-33) Gazeti Biblical Archeology Review linasema hivi: “Mikataba ya uchungaji kama ile iliyofanywa kati ya Labani na Yakobo huenda ilitumika sana miongoni mwa waandishi wa kale na wasomaji wa maandishi ya Biblia.”

Maandishi ya mikataba ya kale iliyochimbuliwa huko Nuzi, Larsa, na sehemu nyinginezo nchini Iraki inaonyesha makubaliano ya namna hiyo. Mkataba ulidumu kuanzia kipindi kimoja cha kunyoa kondoo hadi kipindi kilichofuata kwa mwaka mmoja. Wachungaji walikubali daraka la kutunza idadi hususa ya wanyama walioorodheshwa kulingana na umri na jinsia. Baada ya mwaka, mmiliki wa mifugo hiyo alipewa kiasi walichokubaliana cha sufu, vitu vinavyotokana na maziwa, mifugo iliyoongezeka na vitu vinginevyo. Mchungaji alipewa ziada yoyote iliyopatikana.

Ongezeko la kundi lilitegemea idadi ya kondoo-jike aliokabidhiwa mchungaji. Kondoo-jike 100 walitarajiwa kuzaa kondoo 80 hivi. Mchungaji angelipia hasara yoyote ambayo huenda ingetokea. Hivyo, alikuwa na sababu nzuri ya kuwatunza vizuri wanyama aliyokabidhiwa.