Hamia kwenye habari

Maria Magdalene Alikuwa Nani?

Maria Magdalene Alikuwa Nani?

Jibu la Biblia

 Maria Magdalene alikuwa mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo. Inaelekea jina lake, Magdalene, lilitokana na mji wa Magdala (huenda Magadan), ambalo lilikuwa karibu na Bahari ya Galilaya. Huenda Maria aliwahi kuishi katika eneo hilo.

 Maria Magdalene alikuwa mmoja kati ya wanawake waliosafiri pamoja na Yesu na wanafunzi wake na kuwategemeza kimwili. (Luka 8:1-3) Alishuhudia Yesu alipokuwa anauawa, na alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumwona Yesu baada ya kufufuliwa.—Marko 15:40; Yohana 20:11-18.

 Je, Maria Magdalene alikuwa kahaba?

 Biblia haisemi kwamba Maria Magdalene alikuwa kahaba. Biblia inataja tu kwamba Yesu alitoa roho waovu saba ndani ya Maria.—Luka 8:2.

 Wazo la kwamba alikuwa kahaba lilitoka wapi? Miaka mingi baada ya kifo chake, watu walidai kwamba alikuwa yule mwanamke ambaye alilowesha miguu ya Yesu kwa machozi na kuifuta kwa nywele za kichwa chake. (Luka 7:36-38) Hata hivyo, hakuna sehemu yoyote katika Biblia inayounga mkono jambo hilo.

 Je, Maria Magdalene alikuwa “mtume wa mitume”?

 Hapana. Kanisa Katoliki linamwita Maria “Mt. Maria Magdalene” na pia “mtume aliyetumwa kwa mitume” kwa sababu alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuwajulisha wanafunzi kwamba Yesu amefufuliwa. (Yohana 20:18) Lakini jambo hilo halimaanishi kwamba alikuwa mtume. Na hakuna mahali ambapo Maandiko yanamwita hivyo.—Luka 6:12-16.

 Biblia ilikamilika mwishoni mwa karne ya kwanza W.K. Hata hivyo, mpaka karne ya sita ndipo wenye mamlaka katika kanisa walipofanya uamuzi wa kumpandisha cheo. Maandishi yaliyoandikwa katika karne ya pili na ya tatu—ambayo si sehemu ya Biblia—yanasema kwamba baadhi ya mitume wa Yesu walimwonea wivu Maria. Habari kama hizo zilizotungwa hazina msingi wowote wa Kimaandiko.

 Je, Maria Magdalene alikuwa mke wa Yesu Kristo?

 Hapana. Biblia inataja moja kwa moja kwamba Yesu alikuwa mseja. a