Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Taya la Mamba

Taya la Mamba

MAMBA ni mnyama mwenye uwezo mkubwa wa kung’ata kwa nguvu zaidi kuliko mnyama mwingine yeyote. Kwa mfano, mamba wa maji ya chumvi wanaopatikana Australia, wanaweza kung’ata kwa nguvu mara tatu zaidi ya simba au simbamarara. Pia, taya la mamba lina uwezo wa hali ya juu wa hisi. Uwezo huo unazidi ule wa ncha ya kidole cha mwanadamu. Hilo linawezekanaje ukizingatia kwamba ngozi ya mamba ina magamba?

Taya la mamba limefunikwa kwa maelfu ya viungo vya hisi. Baada ya kufanya uchunguzi, mtafiti Duncan Leitch aliandika hivi: “Kila neva imeunganishwa na fuvu la kichwa.” Mpangilio huo unalinda nyuzi za neva zilizo katika taya na kufanya sehemu fulani za taya ziwe na uwezo mkubwa wa kuhisi. Kwa sababu ya kuwa na uwezo huo, mamba anaweza kutofautisha mdomoni mwake kati ya chakula na uchafu. Hilo pia linamwezesha mamba jike kubeba watoto wake kwa kutumia mdomo bila kuwaua. Taya la mamba lina uwezo mkubwa wa kung’ata kwa nguvu na uwezo mkubwa wa hisi.

Una maoni gani? Je, taya la mamba lilijitokeza lenyewe? Au lilibuniwa?