Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matibabu Mengine Badala ya Kutia Damu Mishipani

Matibabu Mengine Badala ya Kutia Damu Mishipani

WATAALAMU wakuu kutoka nchi zaidi ya 40 walikusanyika huko Moscow kwa ajili ya Kongamano la 60 la Kimataifa la Sosaiti ya Ulaya ya Upasuaji wa Moyo na wa Mishipa katika mwezi wa Mei 20-22, 2011. “Tukio kama hilo ni la maana sana kwa madaktari kama vile Olimpiki ilivyo kwa wanamichezo,” akasema mwanahabari mmoja wa kituo fulani cha televisheni cha Urusi.

Kibanda kilichowavutia watu wengi katika siku zote tatu za kongamano hilo kilikuwa kile kilichotoa habari kuhusu matibabu mengine badala ya kutia damu mishipani. Kibanda hicho kilikuwa cha Huduma za Habari za Hospitali kwa ajili ya Mashahidi wa Yehova. Madaktari walichukua vitabu, DVD, faili nyingi sana zenye habari, na makala za kitiba kuhusu jambo hilo muhimu kutoka katika kibanda hicho. Walipendezwa hasa na DVD iliyokuwa na video yenye kichwa Transfusion-Alternative Strategies—Simple, Safe, Effective. *

Madaktari wengi waliotembelea kibanda hicho walikubali kwamba kuna uhitaji wa kupunguza damu inayovuja wakati wa upasuaji. Mpasuaji wa moyo kutoka Italia aliyetoa hotuba katika kongamano hilo alisema kwamba anawafahamu vizuri Mashahidi wa Yehova na kwamba alikuwa amewafanyia upasuaji wa moyo wagonjwa 70 hivi ambao ni Mashahidi wa Yehova bila kuwatia damu. Pia alisema kwamba katika kliniki yake ni jambo la kawaida kufanya upasuaji bila kuwatia wagonjwa damu. Profesa katika Deutsches Herzzentrum Berlin (Taasisi ya Moyo ya Berlin Ujerumani) alichukua nakala yake ya DVD hiyo na akachukua nyingine kwa ajili ya daktari mwenzake. Aliwaambia wasikilizaji kwamba hivi karibuni alikuwa amemfanyia upasuaji mtoto aliye na uzito wa kilogramu 2.5 tu bila kumtia damu; na kliniki yake imewafanyia upasuaji wa moyo watoto walio na uzito mdogo zaidi ya huo.

Mwezi mmoja baada ya kongamano hilo la Moscow, madaktari kutoka nchi kadhaa walihudhuria Kongamano la Nne la Belomorsk la Madaktari wa Unusukaputi na Madaktari wa Wagonjwa Mahututi Katika Eneo la Kaskazini-magharibi la Urusi, katika jiji la Arkhangel’sk. Kibanda cha Huduma za Habari za Hospitali kiliwekwa katika kongamano hilo pia na kwa mara nyingine kikawavutia watu sana. Daktari mmoja kutoka St. Petersburg alipoona habari zilizokuwa zimewekwa hapo alisema hivi kwa msisimko, “Hizi ndizo habari tunazohitaji!” Alieleza masikitiko yake kwamba kwa sababu ya mazoea, baadhi ya madaktari wenzake huendelea kuwatia damu mishipani wagonjwa waliopata majeraha ya moto. Aliongezea hivi kwa msisimuko, “Hizo habari zenu zitakuwa na faida kubwa katika kongamano kuhusu matibabu ya wagonjwa waliopata majeraha ya moto linalopangiwa kufanywa huko St. Petersburg.”

Kotekote ulimwenguni, madaktari wengi wanazidi kuona faida za kutumia matibabu na upasuaji usiohusisha damu. Baada ya muda tutajua ikiwa matibabu hayo yatakuja kuonwa kuwa matibabu bora zaidi ulimwenguni.

^ fu. 3 Imetolewa na Mashahidi wa Yehova.