Hamia kwenye habari

Hakimu na wawakilishi wa kisheria katika Mahakama ya Wilaya ya Oslo nchini Norway kesi ilipokuwa ikiendelea

MACHI 28, 2024
NORWAY

Mashahidi wa Yehova Wakata Rufaa Dhidi ya Uamuzi Unaopingana na Katiba Nchini Norway

Mashahidi wa Yehova Wakata Rufaa Dhidi ya Uamuzi Unaopingana na Katiba Nchini Norway

Machi 4, 2024, Mahakama ya Wilaya ya Oslo imeunga mkono uamuzi wa serikali ya Norway wa kufuta usajili wa kisheria wa dini ya Mashahidi wa Yehova.

Mwonekano wa nje wa Mahakama ya Wilaya ya Oslo

Gavana wa Jimbo la Oslo na Viken alifuta usajili wa dini yetu mwishoni mwa mwaka 2022. Desemba 30, 2022, Mahakama ya Wilaya ya Oslo ilisitisha kufutwa kwa usajili huo ili kufanya uchunguzi zaidi. Kufikia sasa, serikali ya nchi hiyo imeamua kwamba itawapa Mashahidi wa Yehova usajili wa kisheria ikiwa tu tutabadili utaratibu uliopo wa kuwatenga watenda-dhambi wasiotubu kutanikoni.

Kwa sababu ya uamuzi huo wa kufuta usajili wa Mashahidi wa Yehova, serikali imeacha kutupatia pesa na misaada mingine lakini bado zaidi ya dini 700 zinaendelea kupewa pesa hizo na serikali. Pia, sasa hatuwezi kuteua wahudumu ambao ni Mashahidi wa Yehova watakaokuwa na mamlaka ya kusajili harusi.

Tunapoendelea kusubiri uamuzi utakaotolewa katika kesi ya rufaa, tutaendelea kusali kwa ajili ya “wafalme na wote wenye vyeo vya juu, ili tuendelee kuishi kwa amani na utulivu na ujitoaji-kimungu kamili.”​—1 Timotheo 2:1, 2.