Hamia kwenye habari

Msaada kwa Wafanyakazi wa Hospitali Wanaokabiliana na Mkazo

Msaada kwa Wafanyakazi wa Hospitali Wanaokabiliana na Mkazo

 Bryn anayeishi Kaskazini mwa Carolina, Marekani ni mshiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali ambayo inashirikiana kwa ukaribu na hospitali mbalimbali ili kushughulikia mahitaji ya wagonjwa ambao ni Mashahidi wa Yehova.

 Kwa sababu ya janga la COVID-19, hospitali nyingi haziruhusu wageni waingie. Bryn alimpigia simu mtu anayesimamia mipango ya kuwaandalia wagonjwa na familia zao faraja ya kiroho katika hospitali moja ili kujua anaweza kufanya nini ili kuwasaidia wagonjwa ambao ni Mashahidi wa Yehova.

 Simu ya Bryn ilielekezwa kwa msaidizi wake. Kwa kuzingatia kwamba wageni hawakuruhusiwa kutembelea hospitali hiyo, Bryn aliwaomba ikiwa wagonjwa ambao ni Mashahidi wangepewa namba yake ya simu ili aweze kuzungumza nao. Ombi lake lilikubaliwa.

 Kisha Bryn akafikiria hali ya wafanyakazi wa hospitali. Akamwambia msaidizi huyo kwamba anathamini kazi ambayo wanafanya na alitumaini kwamba walikuwa na afya nzuri. Kisha akasema kwamba amesoma jinsi watu wengi hasa wafanyakazi wa hospitali wanavyokabili mkazo mwingi unaosababishwa na ugonjwa wa virusi vya corona.

 Msaidizi huyo alisema kwamba ugonjwa wa corona umewafanya maisha yao yawe na mkazo mwingi sana.

 Kisha Bryn akasema: “Tovuti yetu ina habari zinazoweza kuwasaidia watu kukabiliana na mkazo. Ikiwa utafungua jw.org na kuandika neno ‘mkazo’ katika sehemu ya Tafuta, utapata makala kadhaa ambazo unaweza kutumia kuwatia moyo wafanyakazi wenzako.”

 Walipokuwa bado wakizungumza, mwanamume huyo aliandika neno “mkazo” kwenye sehemu ya Tafuta na kuona makala zilizopo. Alifurahi sana na kusema: “Nitamwonyesha msimamizi wangu tovuti hii. Habari hizi zitawasaidia wafanyakazi wenzetu na watu wengine. Nitachapisha nakala kadhaa ili nizigawe.”

 Baada ya majuma kadhaa, Bryn alizungumza na msimamizi wa idara hiyo, naye alisema kwamba waliingia kwenye tovuti na kuchapisha nakala kadhaa zilizohusu mkazo na mambo mengine yanayohusiana na mkazo. Waliwapa wauguzi na wafanyakazi wengine hospitalini.

 Bryn anasema hivi: “Msimamizihuyo alinishukuru kwa kazi yetu na kwa makala hizo zilizoandikiwa vizuri. Alisema zimewasaidia sana.”