Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Rekodi za Kale Zathibitisha Kuwepo kwa Kabila Fulani la Israeli

Rekodi za Kale Zathibitisha Kuwepo kwa Kabila Fulani la Israeli

 Biblia inasema kwamba Waisraeli walipomiliki Nchi ya Ahadi na kuigawa kati ya makabila ya Israeli, koo kumi za kabila la Manase zilipata urithi magharibi mwa eneo la Yordani, ambao ulikuwa sehemu tofauti na urithi wa kabila lote. (Yoshua 17:1-6) Je, kuna uthibitisho wa kiakiolojia kwamba hilo lilitukia?

 Mwaka wa 1910 mkusanyo fulani wa vigae uliokuwa na maandishi ulichimbuliwa katika eneo la Samaria. Vigae hivyo, au ostraca, vilikuwa na habari zilizoandikwa katika Kiebrania, ambazo zilionyesha kuletwa kwa bidhaa za kifahari—zilizotia ndani divai na mafuta—kwenye makao ya kifalme katika jiji kuu. Kwa ujumla, vigae au ostraca 102 vilipatikana vinavyokadiriwa kuwa vya karne ya nane K.W.K., lakini ni vigae 63 tu vinavyosomeka kikamili. Hata hivyo, vigae hivyo 63 kwa pamoja vinaonyesha tarehe na majina ya koo, pamoja na watu walioagiza na kupokea bidhaa mbalimbali.

 Inapendeza kujua kwamba koo zote zilizotajwa katika Ostraca za Samaria zilikuwa za kabila la Manase. Kulingana na kitabu kimoja cha marejeo (NIV Archaeological Study Bible), uvumbuzi huo unaandaa “uthibitisho usio wa Biblia kati ya koo za Manase na maeneo ambayo Biblia inasema koo hizo zilirithi.”

Maandishi haya yanamtambulisha mwanamke anayeitwa Noah aliyekuwa mzao wa Manase

 Ostraca za Samaria pia zinathibitisha usahihi wa maneno ya mwandikaji wa Biblia, Amosi, ambaye alisema hivi kuhusu matajiri wa siku zake: “Wanakunywa divai iliyojazwa kwenye mabakuli na kujitia wenyewe mafuta yaliyo bora.” (Amosi 6:1, 6) Ostraca za Samaria zinathibitisha kwamba bidhaa hizo ziliagizwa katika eneo hilo la nchi lililomilikiwa na koo kumi za Manase.