Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Military equipment: Anton Petrus/Moment via Getty Images; money: Wara1982/iStock via Getty Images Plus

ENDELEA KUKESHA!

Matrilioni Yatumiwa Katika Vita—Gharama Halisi Ni Ipi?

Matrilioni Yatumiwa Katika Vita—Gharama Halisi Ni Ipi?

 Gharama ya vita ni kubwa sana.

  •    “Matumizi ya vita yamefikia dola trilioni 2.2 katika vita mbalimbali ulimwenguni pote. Kiwango hicho hakijawahi kufikiwa wakati mwingine wowote.”​—The Washington Post, Februari 13, 2024.

 Hata hivyo, gharama zinatia ndani mengi zaidi ya pesa. Fikiria mfano mmoja tu: Vita nchini Ukrainia.

  •    Wanajeshi. Wataalamu fulani wanakadiria kwamba wanajeshi 500,000 hivi wameuawa au kujeruhiwa tangu vita hivyo vilipoanza miaka miwili iliyopita.

  •    Raia. Zaidi ya watu 28,000 wamekufa au kujeruhiwa, kulingana na Umoja wa Mataifa. Ofisa mmoja wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa alisema hivi: “Haiwezekani kuhesabu ni maisha ya raia wengi kadiri gani ambayo yameharibiwa na vita hivi.” a

 Wanadamu wamelazimika kuteseka sana kutokana na vita ulimwenguni pote.

  •    Milioni 114. Idadi ya watu waliolazimika kuondoka makwao kwa sababu ya vita na jeuri ulimwenguni pote kuanzia Septemba 2023.

  •    Milioni 783. Idadi ya watu wanaokabili njaa kali. “Vita ndicho kisababishi kikubwa zaidi cha njaa, kwa kuwa asilimia 70 ya watu wenye njaa ulimwenguni pote wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na vita na jeuri.”​—Shirika la Chakula Ulimwenguni.

 Je, vita vitakwisha? Kuna tumaini gani la kupata amani? Je, kuna wakati mali zilizopo duniani zitasaidia kuondoa njaa na umaskini? Biblia inasema nini?

Wakati wa vita

 Biblia ilitabiri kutakuwa na vita kila mahali duniani na kuifafanua kuwa mpanda-farasi wa mfano.

  •    “Mwingine akatokea, farasi mwenye rangi ya moto, na yule aliyeketi juu yake akapewa ruhusa ya kuondoa amani duniani ili wauane, naye akapewa upanga mkubwa.”​—Ufunuo 6:4.

 Mpanda-farasi huyo anafuatwa na wengine wawili wanaowakilisha njaa na kifo kinachosababishwa na magonjwa hatari au matatizo mengine. (Ufunuo 6:5-8) Ili kujifunza mengi zaidi kuhusu unabii huo wa Biblia na kwa nini tunaweza kuwa na uhakika unatimizwa leo, soma makala yenye kichwa “Wapanda Farasi Wanne—Jinsi Wanavyokuhusu?

Wakati ujao wenye amani

 Hivi karibuni, utajiri wa ulimwengu huu hautatumiwa tena kwa ajili ya vita. Hata hivyo, hilo halitatokea kwa sababu ya jitihada za wanadamu. Biblia inasema hivi:

  •    Mungu ‘atakomesha vita katika dunia yote.’​—Zaburi 46:9.

  •    Mungu ataondoa madhara yaliyosababishwa na vita. “Atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.”​—Ufunuo 21:4.

  •    Mungu atahakikisha kuna amani ya kudumu kwa ajili ya wote. “Watu wangu watakaa katika makao ya kudumu yenye amani, katika makao salama na mahali pa kupumzika penye utulivu.”​—Isaya 32:18.

 Kulingana na unabii wa Biblia, vita na matukio mengine tunayoona leo yanaonyesha kwamba amani itakuja hivi karibuni.

 Mungu ataletaje wakati ujao wenye amani? Atatumia serikali ya mbinguni, au Ufalme. (Mathayo 6:10) Ili ujifunze Ufalme huo ni nini na utafanya nini kwa ajili yako, tazama video fupi yenye kichwa Ufalme wa Mungu Ni Nini?

a Miroslav Jenca, katibu mkuu msaidizi wa Ulaya wa Umoja wa Mataifa, Desemba 6, 2023.