Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wayahudi ‘walitoka kila taifa kati ya yale yaliyo chini ya mbingu’ ili kuja Yerusalemu katika Pentekoste ya mwaka wa 33 W.K.?

Mtaa uliofurika watu jijini Yerusalemu katika Pentekoste 33 W.K.

Pamoja na simulizi la Matendo 2:5-11, mwandishi Myahudi Philo aliyeishi katika kipindi hicho aliandika simulizi linalofafanua umati wa watu waliokuja Yerusalemu katika Pentekoste ya mwaka wa 33 W.K.

Kuhusu watu waliosafiri kuja Yerusalemu, Philo aliandika hivi: “Umati mkubwa kutoka miji mingi sana huja kwa ajili ya kila sherehe, wengine kupitia nchi kavu, wengine kupitia bahari, kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.” Pia alinukuu barua ambayo Agripa wa Kwanza, mjukuu wa Herode Mkuu, alimwandikia Kaligula, Maliki wa Roma. Katika barua hiyo, Agripa alisema hivi kuhusu Yerusalemu: “Jiji Takatifu . . . si jiji kuu la nchi ya Yudea peke yake bali pia la nchi nyingine nyingi, kwa sababu ya wenyeji wengi wa eneo hilo waliohamia katika nchi jirani.”

Agripa aliorodhesha maeneo ambayo Wayahudi walihamia, yaliyotia ndani sehemu za mbali sana za Mesopotamia, Afrika Kaskazini, Asia Ndogo, Ugiriki, na visiwa vya Mediterania. “Ingawa orodha hiyo haitaji safari za kwenda Yerusalemu,” anasema msomi Joachim Jeremias, “tunajua walifanya hivyo kwa kuwa ilikuwa takwa kwa Wayahudi wote ambao ni watu wazima kwenda huko ili kuabudu.”—Kumbukumbu la Torati 16:16.

Maelfu ya watu waliokuja Yerusalemu kwa ajili ya sherehe za Kiyahudi walikaa wapi?

Mabaki ya kidimbwi cha kuoga kwa ajili ya ibada ya huko Yerusalemu

Sikukuu tatu zilifanywa kila mwaka jijini Yerusalemu—Pasaka, Pentekoste, na Sherehe ya Vibanda. Katika karne ya kwanza, watu wengi kutoka Israeli yote na kila nchi ambayo Wayahudi waliishi, walisafiri hadi Yerusalemu kwa ajili ya sherehe hizo. (Luka 2:41, 42; Matendo 2:1, 5-11) Watu hao wote walihitaji kupata mahali pa kukaa.

Baadhi yao walilala kwa marafiki; wengine katika nyumba za wageni au nyumba za kupanga. Watu wengi walilala kwenye mahema karibu au pembeni mwa kuta za jiji. Yesu alipotembelea Yerusalemu kwa mara ya mwisho, alilala katika jiji la Bethania lililokuwa karibu.Mathayo 21:17.

Majengo kadhaa yenye vidimbwi vya kuogea yamepatikana karibu na hekalu. Inadhaniwa kwamba majengo hayo yalikuwa hoteli ambazo wale waliotembelea Yerusalemu walifikia na kujisafisha kabla ya kuingia hekaluni. Maandishi yaliyochongwa katika jengo moja kati ya hayo yanaonyesha kwamba Theodotus, kuhani na kiongozi wa sinagogi, “alijenga sinagogi ili Torati isomwe humo na . . . pia, hoteli, na vyumba, na mfumo wa maji kwa ajili ya matumizi ya wageni.”