Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Miaka na miezi ilihesabiwaje katika nyakati za Biblia?

KWA Wayahudi walioishi katika Nchi ya Ahadi, mwaka mpya usio wa kidini ulianza kwa kulima na kupanda, shughuli iliyofanywa katika kipindi ambacho kwa sasa ni mwezi wa Septemba/Oktoba.

Kalenda inayotegemea mwezi halisi, yenye miezi 12 (ambapo kila mwezi una siku 29 au 30) ilitokeza mwaka mfupi ikilinganishwa na kalenda ya mwaka inayotegemea jua. Mbinu mbalimbali zimetumiwa ili kupatanisha kalenda hizo mbili. Hilo linaweza kufanywa kwa kuongeza siku za ziada au pindi kwa pindi kuongeza mwezi mmoja, labda kabla ya mwaka unaofuata kuanza. Mfumo huo unapatanisha kalenda na majira ambayo watu walipanda au kuvuna mazao.

Hata hivyo, katika siku za Musa, Mungu aliwaambia watu wake kwamba mwaka wa kidini ungeanza na mwezi wa Abibu, au Nisani, ambao leo ni sawa na mwezi wa Machi/Aprili. (Kut. 12:2; 13:4) Sherehe iliyofanywa katika mwezi huo ilihusisha mavuno ya shayiri.​—Kut. 23:15, 16.

Msomi Emil Schürer, anasema hivi katika kitabu chake The History of the Jewish People in the Age of Jesus Christ, (175 B.C.–A.D. 135): “Sheria ambayo ilitumiwa kuamua ikiwa mwezi ungeongezwa au la ilikuwa rahisi sana. Sikuzote ilikuwa lazima sherehe ya Pasaka, ambayo iliadhimishwa wakati wa mwezi mpevu katika mwezi wa Nisani (Nisani 14), ifanywe baada ya sikusare ya wakati wa majira ya kuchipua . . . Kwa hiyo, ikiwa mwishoni mwa mwaka ingeonekana kwamba siku ya Pasaka ingeangukia kabla ya sikusare ya wakati wa majira ya kuchipua, mwezi [wa 13] ungeongezwa kabla ya mwezi wa Nisani.”

Mashahidi wa Yehova wanazingatia sheria hiyo wanapoamua tarehe inayofaa kuadhimisha Mlo wa Jioni wa Bwana, tukio linalofanywa katika majira ya kuchipua na siku inayolingana na Nisani 14 kwenye kalenda ya Kiebrania. Makutaniko ulimwenguni pote hujulishwa tarehe hiyo mapema. a

Lakini Wayahudi walijuaje mwezi ulipoisha, na mwezi mpya kuanza? Leo, unaweza kutazama kalenda iliyochapishwa au kalenda iliyo kwenye kifaa chako cha kielektroni. Hata hivyo, katika nyakati za Biblia, haikuwa rahisi hivyo.

Katika kipindi cha Gharika, miezi ilikuwa na urefu wa siku 30. (Mwa. 7:11, 24; 8:3, 4) Baadaye, miongoni mwa Wayahudi mwezi wa kalenda haukuwa tu na siku 30. Katika kalenda ya Kiyahudi, mwezi wa kalenda ulianza mara tu mwezi mpya ulipoonekana. Mwezi huo mpya ungeonekana siku 29 au 30 baada ya mwezi uliotangulia kuanza.

Pindi moja, Daudi na Yonathani waliurejelea mwezi wakisema: “Kesho ni mwezi mpya.” (1 Sam. 20:5, 18) Hivyo, inaonekana kufikia karne ya 11 K.W.K., miezi ilihesabiwa mapema kabla haijaanza. Mwisraeli wa kawaida angetambuaje mwezi mpya ulipoanza? Mishna, mkusanyo wa sheria ya mdomo na desturi za Kiyahudi, inatoa habari fulani. Inaonyesha kwamba baada ya Waisraeli kutoka uhamishoni, Sanhedrini (mahakama kuu ya Kiyahudi) ilihusika. Katika kipindi cha miezi saba ambapo sherehe zilifanywa, mahakama iliketi katika siku ya 30 ya mwezi. Wanaume hao walikuwa na jukumu la kuamua mwezi unaofuata ungeanza lini. Waliamua kwa kutegemea nini?

Wanaume waliowekwa kwenye sehemu zilizoinuka kuzunguka Yerusalemu walitazama anga la usiku ili waweze kutambua mara tu mwezi mpya ulipoonekana. Na haraka wangeijulisha Sanhedrini. Wanaume wa mahakama hiyo walipokuwa na ushahidi wa kutosha kwamba mwezi mpya umeonekana, walitangaza kuanza kwa mwezi mpya. Namna gani ikiwa mawingu au ukungu ungewazuia watazamaji kuona mwezi mpya? Basi mwezi uliokuwa unaendelea ungetangazwa kuwa na siku 30, na mwezi mpya ungeanza.

Mishna inaeleza kwamba uamuzi wa Sanhedrini ulitangazwa kwa ishara ya moto uliowashwa juu ya Mlima wa Mizeituni, karibu na Yerusalemu. Katika maeneo mengine yaliyoinuka kotekote Israeli, mioto mikubwa iliwashwa ili kueneza habari hizo. Katika pindi za baadaye, wajumbe wangetumwa kutoa taarifa. Hivyo, Wayahudi walioishi Yerusalemu, kotekote Israeli, na maeneo mengine walijulishwa kuanza kwa mwezi mpya. Hivyo, wote wangeweza kuadhimisha sherehe za majira mbalimbali wakati uleule.

Chati iliyoambatanishwa inaweza kukusaidia kuelewa miezi, sherehe, na majira ya kalenda ya Kiebrania.

a Tazama gazeti la Mnara wa Mlinzi la Februari 15, 1990, uku. 15, na Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika toleo la Kiingereza la Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 1977.