Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Alishikamana na Imani Yake

Alishikamana na Imani Yake

Song Hee alipokuwa na umri wa miaka 11, mama yake aligundua kwamba mgongo wa binti yake umepinda. Daktari aligundua kwamba ana ugonjwa wa mgongo uliopinda, yaani uti wake wa mgongo umepinda kama herufi “C” au “S.” Hali ya Song Hee ilizidi kuwa mbaya kiasi cha kwamba alihitaji kufanyiwa upasuaji. Hata hivyo, Song Hee alikataa kutiwa damu mishipani. Gazeti la “Amkeni” lilimhoji Song Hee.

Je, madaktari waliweza kukusaidia ulipogunduliwa na ugonjwa huo?

Ijapokuwa kwa miaka mitatu hivi, nilikuwa chini ya uangalizi wa madaktari wawili, bado uti wangu wa mgongo ulizidi kupinda. Hali ilikuwa mbaya sana kiasi cha kwamba uti wa mgongo ukaanza kusonga moyo na mapafu yangu na kufanya iwe vigumu kupumua. Nilihitaji kufanyiwa upasuaji.

Je, ulikubali kufanyiwa upasuaji?

Ndiyo. Hata hivyo, niliambiwa kwamba upasuaji huo haungekuwa rahisi. Kufikia wakati huo, uti wangu wa mgongo ulipinda kufikia nyuzi 116, kiwango ambacho ni hatari sana kwa afya. Pia, kufanyiwa upasuaji kulitokeza changamoto moja ya pekee. Kwa sababu ya imani yangu inayotegemea Biblia, mimi nisingekubali kutiwa damu mishipani. *

Je, ulipata daktari aliyekuwa tayari kukutibu?

Mimi na mama yangu tulimpata daktari mmoja katika jimbo tulioishi la Florida, Marekani. Hata hivyo, nilipomwambia kwamba ningependa kufanyiwa upasuaji bila kutiwa damu, alisema kwamba hakuna daktari mpasuaji ambaye angekubali kufanya upasuaji huo mgumu bila kunitia damu. Pia, aliniambia kwamba huenda ningekufa kabla ya kufikisha umri wa miaka 20 ikiwa sitafanyiwa upasuaji. Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 14.

Je, ulimwambia msingi wa imani yako?

Ndiyo. Nilimwambia kwamba imani yangu inategemea Biblia, na kwamba Mungu anaiona damu kuwa takatifu iwe ya mwanadamu au mnyama. * Mwisraeli angeuawa ikiwa angekula damu! * Nilimwonyesha pia andiko la Matendo 15:19, 20. Kwa sehemu, andiko hilo linawaagiza hivi Wakristo: ‘Jiepusheni . . . na damu.’ Hilo linamaanisha kwamba damu haipaswi kuwekwa katika mwili wa mtu kwa njia yoyote ile, iwe kwa kutiwa mishipani au kuliwa.

Daktari mpasuaji alisemaje?

Aliendelea kusisitiza kwamba bado angehitaji kunitia damu mishipani. Nilishangazwa pia kwamba hospitali ilisema, ikiwa ningekubali kutiwa damu, nisingelipia gharama za upasuaji.

Hiyo ilikuwa nafasi nzuri! Wewe na mama yako mlifanya nini?

Ingawa hakuna mtu aliyekuwa tayari kufanya upasuaji bila damu, tuliazimia kushikamana na imani yetu. Mambo yakawa magumu hata zaidi. Kulingana na sheria, nilikuwa bado mtoto. Kwa kuwa hali ya afya yangu ilizidi kuwa mbaya, kesi yangu ilipelekwa mahakamani. Hata hivyo, tulishukuru sana wakili wa jimbo la Florida alipotupatia siku 30 za kutafuta daktari mpasuaji atakayekubali kufanya upasuaji bila damu.

Je, mlipata daktari?

Ndiyo! Kwa fadhili, Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali (HLC) ya Mashahidi wa Yehova iliyo katika jimbo letu iliwasiliana na mtaalamu wa kutibu ugonjwa wa mgongo uliopinda katika jimbo la New York aliyekuwa mtazamo tofauti na aliyekubali kuniona. Hivyo, tuliweza kutii amri ya mahakama. *

Matokeo yalikuwaje baada ya kufanyiwa upasuaji?

Upasuaji ulifanikiwa! Ili kunyoosha uti wa mgongo wangu, Daktari Robert M. Bernstein, aliingiza katika mgongo wangu vyuma vidogo vinavyoweza kurekebishwa. Alinifanyia upasuaji mara mbili katika kipindi cha majuma manne.

Kwa nini alifanya upasuaji kwa hatua mbili?

Ikiwa kwa sababu ya upasuaji wa mara ya kwanza ningepoteza damu nyingi sana, kipindi cha majuma mawili kingefaa kuupa mwili wangu muda wa kuzalisha chembe nyekundu za damu kabla ya kufanyiwa upasuaji wa pili. Hata hivyo, katika upasuaji wote huo, nilipoteza damu kidogo. Ninaishukuru timu ya madaktari wapasuaji waliokuwa na mipango mizuri, ustadi, na uangalifu mkubwa. Nilipona vizuri bila kuwa na matatizo yoyote ambayo huenda ningepata ikiwa ningetiwa damu mishipani. *

Daktari aliyekufanyia upasuaji alihisije baada ya kuona hali yako?

Madaktari wanapaswa kufikiria kikamili hali ya mgonjwa

Alifurahi sana! Alisema hivi: “Matibabu si kufanya upasuaji tu.” Aliendelea kusema kwamba anahisi kwamba madaktari wanapaswa kufikiria kikamili hali ya mgonjwa kutia ndani imani na viwango vyake. Watu wengine ambao si Mashahidi wa Yehova, wanakubaliana na maoni hayo.

^ fu. 7 Mama ya Song Hee ni Shahidi wa Yehova. Song Hee pia ni Shahidi wa Yehova na alibatizwa mwaka wa 2012, akiwa na umri wa miaka 16.

^ fu. 17 Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali huwasaidia Mashahidi walio wagonjwa kutafuta madaktari walio tayari kuwatibu bila kutumia damu.

^ fu. 21 Katika makala yake kuhusu madhara ya kutiwa damu mishipani, Clinical Excellence Commission New South Wales (Australia) Health, inasema hivi: “Kutiwa damu mishipani ni sawa na kupandikiza tishu iliyo hai katika mwili. Kwa asili, mwili wa binadamu hukataa kitu chochote kipya kinachowekwa katika mwili. Ni muhimu sana kulinda hali njema ya mwili.”