Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Alibatrosi Anayeruka Bila Kupoteza Nishati Nyingi

Alibatrosi Anayeruka Bila Kupoteza Nishati Nyingi

NDEGE ambao hupaa juu sana wana uwezo wa kuendelea kuruka bila kutumia nguvu nyingi. Mfano mmoja ni alibatrosi aina ya wandering. Mabawa ya ndege huyo yana urefu wa mita 3.4 kutoka ncha moja hadi ile nyingine na uzito wa kilogramu 8.5, na kwa sababu hiyo ndege huyo anaweza kusafiri umbali wa maelfu ya kilomita bila kutumia nishati nyingi! Anafaulu kufanya hivyo kwa sababu ya umbo la mwili wake na mbinu anayotumia kupaa.

Fikiria hili: Anaposafiri, alibatrosi hutumia kano fulani ya pekee. Kano hiyo humsaidia ndege huyo kushikilia mabawa yake anapoyakunjua kabisa na hivyo kuruhusu misuli ipumzike. Mbinu nyingine inayomsaidia kuendelea kupaa kwa saa nyingi inahusisha kutumia upepo unaopiga kutoka baharini.

Wanapokuwa juu ya bahari, alibatrosi hupaa, hugeuka, na kushuka wakijipindapinda kwa njia ileile—mbinu inayompa ndege huyo mwendo wa kutosha kulipia mwendo anaopoteza kutokana na upepo unaompiga. Wanasayansi waligundua hivi majuzi tu jinsi ndege huyo anavyofanya hivyo. Wakitumia vifaa vya hali ya juu vya kutambua mahali alipo na programu za pekee za kompyuta, waligundua kwamba alibatrosi hupata nishati anayohitaji anapoacha kusonga dhidi ya upepo na badala yake kuanza kufuata mkondo wa upepo. Wanasayansi wanasema kwamba ndege hao huendelea kutumia mbinu hiyo ya kupokea nishati kutoka kwa upepo. Matokeo ni nini? Ndege huyo anaweza kupaa kwa saa nyingi bila kutua na hata bila kupiga mabawa yake!

Huenda utafiti huo ukawasaidia mainjinia kubuni ndege zinazoweza kupaa bila kutumia mafuta mengi, na labda hata zinazoweza kupaa bila kutumia injini.

Una maoni gani? Je, uwezo wa alibatrosi wa kuruka bila kupoteza nishati, kutia ndani mwili wake wa pekee, ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?