Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HABARI KUU

Jinsi ya Kujilinda na Magonjwa

Jinsi ya Kujilinda na Magonjwa

Kila siku mwili wako hupambana na maadui wengi hatari wasioonekana. Maadui hao ni kama vile bakteria, virusi, na vimelea, nao ni hatari kwa afya yako. * Huenda usijue chochote kuhusu mapambano hayo, kwa sababu maadui wengi huzuiwa au kuuawa na mfumo wako wa kinga kabla ya kuonekana kwa dalili yoyote. Hata hivyo, nyakati fulani maadui hao hushinda nguvu kinga za mwili wako. Hivyo, utahitaji kutumia dawa au matibabu mengine ili kuwashinda maadui hao.

Kwa maelfu ya miaka, watu hawakujua vizuri hatari za vimelea na bakteria fulani wenye madhara. Hata hivyo, katika karne ya 19 wanasayansi walipothibitisha kwamba kuna uhusiano kati ya magonjwa na vimelea, tulielewa vizuri jinsi tunavyoweza kujilinda. Tangu wakati huo, wataalamu wa tiba wamejitahidi kutokomeza au kupunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi ya magonjwa fulani, kutia ndani ugonjwa wa ndui na polio. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni magonjwa mengine, kama vile homa ya manjano na kidingapopo, yamerudi tena. Kwa nini? Fikiria sababu zifuatazo:

  • Kila mwaka, mamilioni ya watu husafiri kotekote duniani, na mara nyingi wao huwa na maambukizi ya vimelea vinavyosababisha magonjwa. Kulingana na makala moja kwenye jarida la Clinical Infectious Diseases, watu wanaosafiri kutoka nchi moja hadi nyingine wanaweza kusambaza “karibu aina zote za magonjwa ya kuambukizwa.”

  • Baadhi ya bakteria hawawezi kuuawa kwa dawa. Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni ilisema: “Ulimwengu unaelekea kipindi ambacho dawa hazitafanya kazi, na hivyo maradhi ya kawaida . . . yatasababisha vifo tena.”

  • Machafuko ya kisiasa na umaskini huzuia jitihada za serikali za kudhibiti kuenea kwa magonjwa.

  • Watu wengi hawajui jinsi wanavyoweza kujilinda dhidi ya magonjwa.

Licha ya hayo, kuna mambo mengi unayoweza kufanya ili kujilinda, wewe na familia yako. Makala inayofuata itazungumzia njia rahisi za kujilinda na magonjwa unazoweza kutumia hata ikiwa unaishi katika nchi inayoendelea.

^ fu. 3 Vimelea vingi havisababishi magonjwa. Makala hizi zitazungumzia hasa vimelea na bakteria ambao ni hatari kwa afya yako.