Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa Kusafisha Antena wa Chungu Aina ya Carpenter

Uwezo wa Kusafisha Antena wa Chungu Aina ya Carpenter

 Usafi ni muhimu kwa mdudu ili aweze kuruka, kupanda, na kutambua mazingira. Kwa mfano, antena chafu hupunguza uwezo wa chungu wa kusafiri, kuwasiliana, na kunusa harufu. Alexander Hackmann, mtaalamu wa kuchunguza wanyama anasema kwamba “huwezi kupata mdudu mchafu. Wamejifunza kukabiliana na uchafu unaopatikana ardhini.”

 Jambo la kufikiria: Hackmann na wafanyakazi wenzake walichunguza jinsi chungu aina ya carpenter (Camponotus rufifemur) anavyosafisha antena yake. Waligundua kwamba chungu huyo huondoa uchafu wa ukubwa mbalimbali kutoka kwenye antena yake kwa kukunja mguu kufanyiza aina fulani ya kibanio, kisha anapitisha kila antena kupitia kibanio hicho. Kwa kufanya hivyo, vipande vikubwa vya uchafu vinaondolewa. Chembe ndogo hutolewa kwa kitu kilicho kama brashi laini yenye mianya iliyo na ukubwa wa vinywele vya antena zake. Kisha chembe ndogo kabisa​—zenye ukubwa wa 1/80 wa kipenyo cha nywele ya mwanadamu​—huondolewa na brashi ndogo zaidi.

 Tazama chungu aina ya carpenter akisafisha antena zake

 Hackmann na kikundi chake wanaamini kwamba njia inayotumiwa na chungu kusafisha antena zake inaweza kutumiwa viwandani. Kwa mfano, njia kama hiyo inaweza kutumiwa kudumisha usafi wakati wa kutengeneza vifaa vya kielektroni vinavyoweza kuathiriwa kwa urahisi na ambavyo vinaweza kuharibika ikiwa vinapatwa hata na uchafu mdogo sana.

 Una maoni gani: Je, uwezo wa chungu wa kusafisha antena ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?