Hamia kwenye habari

MSAADA KWA AJILI YA FAMILIA

Nifanye Nini Ikiwa Mtoto Wangu Anaonewa?

Nifanye Nini Ikiwa Mtoto Wangu Anaonewa?

 Mwana wako anasema kwamba anaonewa na wenzake shuleni. Utafanya nini? Je, uwaambie walimu wamwadhibu mwanafunzi anayemwonea? Au umfundishe mwana wako kupigana ili ajitetee? Kabla ya kuamua, fikiria mambo fulani kuhusu uonevu. a

 Ninapaswa kujua nini kuhusu uonevu?

 Uonevu ni nini? Uonevu ni unyanyasaji wa kimwili au wa kihisia unaofanywa kimakusudi na unaoendelea. Hivyo, si kila wakati mtu anapotukanwa au kutendewa kikatili anaweza kusema kwamba ameonewa.

 Kwa nini ni muhimu kujua kihususa maana ya uonevu? Kwa sababu watu fulani hufikiri “uonevu” ni tendo lolote linalokusumbua, hata liwe dogo kadiri gani. Lakini unapolalamika kwa sababu ya mambo madogo, utamfundisha mtoto wako kwamba hawezi kutatua matatizo​—na huo ni uwezo ambao anahitaji sasa na atahitaji atakapokuwa mtu mzima.

 Kanuni ya Biblia: “Usikasirike haraka.”​—Mhubiri 7:9.

 Jambo kuu: Ingawa huenda ukahitaji kuingilia visa fulani, huenda hali nyingine zikampa mtoto wako nafasi ya kusitawisha uvumilivu na kumsaidia kujifunza jinsi ya kushughulika na watu.—Wakolosai 3:13.

 Vipi mtoto wako akisema kwamba ananyanyaswa kwa kuendelea na kimakusudi?

 Ninaweza kusaidiaje?

  •   Msikilize kwa subira. Jaribu kuamua (1) ni nini kinachompata na (2) kwa nini yeye ndiye anayeonewa. Usikate kauli kabla ya kupata habari kamili. Jiulize, ‘Je, kunaweza kuwa na mambo yanayoendelea ambayo sifahamu?’ Ili upate habari kamili, huenda ukahitaji kuzungumza na mwalimu wa mtoto wako au wazazi wa yule mtoto mwingine.

     Kanuni ya Biblia: “Yeyote anayejibu kabla ya kusikia ukweli wa mambo, huo ni upumbavu na aibu kwake.”​—Methali 18:13.

  •   Ikiwa kweli mtoto wako anaonewa, msaidie atambue kwamba jinsi anavyozungumza na kutenda kunaweza kurekebisha mambo au kuyafanya yawe mabaya zaidi. Kwa mfano, Biblia inasema hivi: “Jibu la upole hutuliza hasira, lakini neno kali huchochea hasira.” (Methali 15:1) Kwa kweli, kulipiza kisasi kunaweza kufanya mambo yawe mabaya kwake, na kuongeza uonevu badala ya kuupunguza.

     Kanuni ya Biblia: “Msilipe ubaya kwa ubaya au matukano kwa matukano.”​—1 Petro 3:9.

  •   Mweleze mtoto wako kwamba kuamua kutolipiza kisasi hakumaanishi kwamba yeye ni dhaifu. Badala yake, kunamfanya awe na nguvu kwa sababu anakataa kudhibitiwa na mtu mwingine. Kwa njia fulani, anamshinda mnyanyasaji bila kuwa mnyanyasaji.

     Ni muhimu kwa mtoto wako kukumbuka hilo anaponyanyaswa kupitia mtandao. Kuanza kubishana na mwonevu kupitia mtandao kutampa ruhusa ya kuendelea, na pia kunaweza kumfanya mtoto wako awe mnyanyasaji! Kwa hiyo, nyakati nyingine jibu bora zaidi ni kutomjibu mnyanyasaji​—mbinu inayoweza kumchanganya na hivyo kumfanya mtoto wako aweze kumdhibiti.

     Kanuni ya Biblia: “Pasipo na kuni moto huzimika.”​—Methali 26:20.

  •   Katika visa fulani, mtoto wako anaweza kuwaepuka watu na maeneo ambayo huenda ikawa rahisi kuonewa. Kwa mfano, ikiwa anajua mahali ambapo mtu au kikundi fulani kitakuwepo, anaweza kuepuka matatizo kwa kutumia njia nyingine.

     Kanuni ya Biblia: “Mtu mwerevu huona hatari na kujificha, lakini wajinga husonga mbele na kupata madhara.”​—Methali 22:3.

Huenda ukahitaji kuzungumza na mwalimu wa mtoto wako au wazazi wa yule mtoto mwingine

 JARIBU KUFANYA HIVI: Msaidie mtoto wako kufikiria faida na madhara yanayoweza kutokea. Kwa mfano:

  •  Huenda nini kikatokea akiamua tu kumpuuza mnyanyasaji?

  •  Namna gani akimwambia kwa uthabiti mnyanyasaji aache kumsumbua?

  •  Vipi akiripoti uonevu huo kwa walimu?

  •  Je, anaweza kumchanganya mnyanyasaji huyo kwa kuwa mwenye urafiki au kwa kutumia ucheshi?

 Iwe uonevu unatokea moja kwa moja au kupitia mtandao, kila hali ni tofauti. Kwa hiyo, msaidie mtoto wako kupata suluhisho linalofaa. Mhakikishie kwamba utamtegemeza katika hali hiyo ngumu.

 Kanuni ya Biblia: “Rafiki wa kweli hupenda nyakati zote naye ni ndugu ambaye amezaliwa kwa ajili ya nyakati za taabu.”​—Methali 17:17.

a Habari zilizo katika makala hii zinawahusu watoto wa kiume na wa kike.