Hamia kwenye habari

MSAADA KWA AJILI YA FAMILIA | WAZAZI

Mambo Ambayo Wazazi Wanapaswa Kujua Kuhusu Kituo cha Kutunzia Watoto Wadogo

Mambo Ambayo Wazazi Wanapaswa Kujua Kuhusu Kituo cha Kutunzia Watoto Wadogo

 Baadhi ya wazazi wanaofanya kazi huamua kupeleka watoto wao ambao hawajaanza kwenda shule katika kituo cha kutunza watoto wadogo—kituo kinachoendeshwa kama shule au darasa. Je, hilo litamfaa mtoto wako?

 Maswali unayopaswa kujiuliza

 Je, kumpeleka mtoto katika kituo hicho kutaathiri uhusiano wetu? Kunaweza. Katika miaka yake ya mwanzoni, ubongo wa mtoto hukua haraka katika njia ambazo huathiri uhusiano wake na watu wengine. Jitahidi kuwa karibu na mtoto wako kadiri uwezavyo katika kipindi hicho cha ukuzi wake.—Kumbukumbu la Torati 6:6, 7.

  •    Wazazi wanaofikiria kumpeleka mtoto wao katika kituo cha kutunzia watoto, wanapaswa kutafakari jinsi watakavyoendelea kudumisha uhusiano wa karibu sana na mtoto wao.

 Je, kumpeleka kutapunguza ushawishi wako kwa mtoto? Kunaweza. “Kadiri watoto ambao hawajaanza shule wanavyokuwa pamoja, ndivyo wanavyozidi kuathiriwa na marafiki wao,” kinasema kitabu Hold On to Your Kids.

  •    Wazazi wanaofikiria kumpeleka mtoto wao katika kituo cha kutunzia watoto, wanapaswa kufikiria ikiwa wataendelea kuwa na ushawishi kwa mtoto wao.

 Je, kituo hicho kitafanya iwe rahisi kwa mtoto wako kujifunza atakapoanza shule? Baadhi ya watu husema ndiyo. Wengine wanasema vituo hivyo vina manufaa kidogo sana katika ukuzi wa mtoto au havina manufaa yoyote. Vyovyote vile, mwanasaikolojia wa watoto, Penelope Leach aliandika hivi: “Usiamini upesi kwamba ‘elimu’ ndio ufunguo wa maisha na eti kadiri mtoto anavyopata elimu mapema zaidi ndivyo atakavyonufaika zaidi. Ukifanya hivyo, utakuwa ukipuuza ‘elimu’ ambayo umekuwa ukimpa mtoto wako tangu alipozaliwa.”

  •    Wazazi wanaofikiria kumpeleka mtoto wao katika kituo cha kutunzia watoto, wanapaswa kufikiria ikiwa kufanya hivyo kuna manufaa au hata ikiwa ni lazima.

 Je, inawezekana kwako au kwa mwenzi wako kukaa nyumbani na kumlea mtoto badala ya kufanya kazi? Katika visa fulani, wazazi wote wawili hufanya kazi ili tu kupata mali zaidi. Je, mali hizo ni muhimu zaidi kuliko mtoto wako?

  •    Wazazi wanaofikiria kumpeleka mtoto wao katika kituo cha kutunzia watoto, wanapaswa kufikiria ikiwa wanaweza kupunguza gharama ili mzazi mmoja abaki nyumbani.

 Uamuzi wa kumpeleka mtoto wenu katika kituo cha kutunzia watoto unapaswa kufanywa baada ya kutafakari kwa makini faida na hasara. Baada ya kufanya hivyo, vipi mkihisi kwamba kumpeleka mtoto wenu katika kituo cha kuwatunzia watoto ndio uamuzi unaofaa kwa familia yenu?

 Unachopaswa kufanya

 Biblia inasema kwamba “mwerevu hutafakari kila hatua.” (Methali 14:15) Ukiwa na kanuni hiyo akilini, tafakari kwa makini kabla ya kuchagua aina yoyote ya kituo cha kutunzia watoto.

 Kuna vituo vya aina gani?

  •   Baadhi ya wazazi wamechagua kituo cha kutunzia watoto kilicho katika nyumba ya mtu ambapo mtu mmoja au watu kadhaa huwatunza watoto wachache.

  •   Wazazi wengine huamua mtu wa ukoo au yaya aishi pamoja nao ili amtunze mtoto wao.

 Njia zote hizo zina faida na hasara. Kwa nini msizungumze na wazazi wengine ambao wametumia huduma za kuwatunza watoto wao? Biblia inasema hivi: “Hekima ni ya wale wanaotafuta ushauri.”—Methali 13:10.

 Vipi mkiamua kumpeleka mtoto wenu katika kituo cha kutunzia watoto? Mkiamua kufanya hivyo basi . . .

 Chunguza kituo hicho

  •   Je, kina leseni au kinasimamiwa kulingana na sheria? Kina sifa au ubora gani?

  •   Je, kituo hicho ni safi na salama?

  •   Kinatoa huduma gani? a

 Wafahamu walezi

  •   Je, wana elimu ya kulea watoto kwa kiwango gani? Hii inaweza kutia ndani elimu ya kufundisha watoto, kutoa huduma ya kwanza, na uwezo wa kusaidia mapigo ya moyo ya mtu yaanze tena ili apumue (CPR).

  •   Je, unaweza kupata taarifa za ziada kuwahusu walezi wa mtoto wako ili kujua ikiwa waliwahi kufanya makosa ya jinai?

  •   Je, wafanyakazi hubadilishwa mara nyingi? Ikiwa wanabadilishwa mara nyingi, hilo litamaanisha kwamba mtoto wako atahitaji kila mara kuanza tena kumzoea mlezi mpya.

  •   Kuna uwiano wa walezi wangapi kwa kila mtoto katika kituo hicho? Ikiwa kuna watoto wengi kuliko walezi, hilo linamaanisha kwamba mtoto wako hatatunzwa ipasavyo. Hata hivyo, utunzaji huo utategemea umri na uwezo wa mtoto wako.

  •   Je, walezi wako tayari kuwasiliana nawe ikiwa una mahangaiko kuhusu mtoto wako—au ikiwa wana mahangaiko?

a Kwa mfano, je, wanatumia televisheni kama mlezi au kuna mazoezi ya akili na mwili yatakayomsaidia mtoto wako?