Hamia kwenye habari

MSAADA KWA AJILI YA FAMILIA | KULEA WATOTO

Watoto na Mitandao ya Kijamii​—Sehemu ya 1: Je, Mtoto Wangu Atumie Mitandao ya Kijamii?

Watoto na Mitandao ya Kijamii​—Sehemu ya 1: Je, Mtoto Wangu Atumie Mitandao ya Kijamii?

 Katika uchunguzi mmoja, asilimia 97 ya vijana walisema kwamba wanatumia mitandao ya kijamii. Je, mtoto wako pia anatamani sana kufanya hivyo? Ikiwa ndivyo, kuna mambo machache unayohitaji kuzingatia.

Katika makala hii

 Mtoto wako atatumiaje wakati wake?

 Tovuti inayoitwa HelpGuide inasema hivi: “Mitandao ya kijamii imebuniwa kwa njia ambayo itanasa uangalifu wako, ikufanye usiondoke mtandaoni, na kukulazimisha kuchunguza kifaa chako kila wakati ili kuona habari za karibuni.”

 “Mimi hukusudia kutumia mitandao ya kijamii kwa dakika chache tu lakini ninakuta nimeitumia kwa saa nyingi. Inaweza kuwa vigumu sana kuweka simu chini na kutafuta kitu muhimu zaidi cha kufanya.”​—Lynne, 20.

 Jiulize: Je, mtoto wangu atakuwa na uwezo wa kujizuia ili kufuata sheria ninazomwekea kuhusu muda anaopaswa kutumia katika mitandao ya kijamii? Je, mtoto wangu amekomaa vya kutosha kujiwekea mipaka na kuifuata?

 Kanuni ya Biblia: “Endeleeni kuangalia sana jinsi mnavyotembea, . . . kama watu wenye hekima, mkiutumia vizuri kabisa wakati wenu.”​—Waefeso 5:15, 16.

Kumruhusu mtoto wako kutumia mitandao ya kijamii bila kumwekea mipaka ni kama kumruhusu apande farasi bila kumfundisha mtoto jinsi ya kufanya hivyo

 Mtoto wako atakuwa na maoni gani kuhusu urafiki?

 Maneno “mitandao ya kijamii” yanadokeza kwamba watumiaji wana marafiki au wanashirikiana na watu wanaowafahamu. Hata hivyo, uhusiano huo si halisi.

 “Nimetambua kwamba vijana wengi wanafikiri kimakosa kwamba watu wengi wakipendezwa na kitu walichopachika mtandaoni au wakiwa na wafuasi wengi, basi hilo linamaanisha kwamba watu wanawapenda sana hata ingawa hawawafahamu watu hao.”​—Patricia, 17.

 Jiulize: Je, mtoto wangu ana ukomavu wa kutosha kujua kwamba kupendwa na watu mtandaoni si jambo muhimu? Je, ana uwezo wa kuanzisha urafiki na watu nje ya mtandao?

 Kanuni ya Biblia: “Rafiki wa kweli hupenda nyakati zote naye ni ndugu ambaye amezaliwa kwa ajili ya nyakati za taabu.”​—Methali 17:17.

 Mtoto wako ataathiriwaje kihisia?

 Watafiti wamegundua kwamba watu wanapotumia mitandao ya kijamii kupita kiasi, mara nyingi wanahisi upweke, wasiwasi, na hata wanashuka moyo.

 “Kuona picha za mambo ambayo marafiki wako wanafanya pamoja na wengine bila wewe kuwepo kunaweza kukufanya uhuzunike.”​—Serena, 19.

 Jiulize: Je, mtoto wangu ana ukomavu utakaomsaidia kuepuka kuwa mbinafsi, mwenye ushindani, au kuathiriwa kwa urahisi na mambo ambayo anaona wengine wakifanya kwenye mtandao wa kijamii?

 Kanuni ya Biblia: “Tusiwe tukijisifu, tusichochee mashindano kati yetu, wala tusioneane wivu.”​—Wagalatia 5:26.

 Mtoto wako atajiendeshaje kwenye mtandao?

 Mtu anapotumia mitandao ya kijamii anaweza kunyanyaswa na wengine kwenye mitandao, au kutumiwa ujumbe mchafu, na kutazama ponografia. Ingawa mtoto wako hakusudii kufanya mambo hayo, kuna uwezekano kwamba atakabiliwa na mambo hayo.

 “Nilitambua kwamba mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii yanaweza kubadilika upesi na kuwa mabaya. Muziki usiofaa na lugha chafu hutumiwa sana.”​—Linda, 23.

 Jiulize: Je, mtoto wangu ana ukomavu wa kutosha utakaomsaidia kutenda kwa njia inayofaa mtandaoni? Je, mtoto wangu atakuwa na uwezo wa kuepuka habari zisizofaa?

 Kanuni ya Biblia: “Uasherati na kila namna ya ukosefu wa usafi au pupa visitajwe kamwe miongoni mwenu, . . . wala mwenendo wa aibu wala maneno ya kipumbavu wala mizaha michafu.”​—Waefeso 5:3, 4.

 Je, ni lazima mtu atumie mitandao ya kijamii?

 Si lazima mtu atumie mtandao wa kijamii ili aendelee kuwa hai au kuwa na maisha yenye starehe na furaha. Vijana wengi wako tayari kuishi bila kutumia mitandao ya kijamii, hata wale ambao wakati fulani waliitumia wakaamua kuiacha.

 “Baada ya kuona jinsi dada yangu alivyoathiriwa vibaya na mitandao ya kijamii, niliamua kuacha kuitumia. Tangu wakati huo, nimekuwa mwenye furaha zaidi na ninahisi kwamba ninafurahia maisha zaidi.”​—Nathan, 17.

 Jambo kuu: Kabla ya kumruhusu mtoto wako kutumia mitandao ya kijamii, hakikisha kwamba ana ukomavu wa kutosha wa kushikamana na mipaka iliyowekwa ya wakati, kudumisha urafiki mzuri, na kuepuka habari zisizofaa.

 Kanuni ya Biblia: “Mwerevu hutafakari kila hatua.”​—Methali 14:15.