Hamia kwenye habari

Walidhani Ni Kasisi

Walidhani Ni Kasisi

Osman, mke wake, na binti yake walikuwa wakihubiri kwa kutumia kigari nje ya eneo la makaburi nchini Chile. Ghafla, kundi kubwa la waombolezaji likawasili huku wakipiga muziki wenye sauti kubwa. Baadhi ya watu hao walidhani kimakosa kwamba Osman alikuwa kasisi wao, basi wakaenda mahali alipokuwa, wakamkumbatia, na kusema kwa msisimko, “Mchungaji, asante kwa kufika mapema, tulikuwa tunakutarajia!”

Ingawa Osman alijaribu kuwaeleza ukweli wa mambo, kundi hilo lenye kelele halikumwelewa. Dakika chache baada ya kundi hilo kuingia kwenye eneo la makaburi, watu wachache walirudi na kusema, “Mchungaji, tunakusubiri makaburini.”

Baada ya kundi hilo kunyamaza, Osman aliwaeleza yeye ni nani na kwa nini alikuwa hapo. Walikasirika kwamba kasisi wao hakuwa amefika, basi wakamuuliza Osman hivi, “Tafadhali unaweza kuingia useme maneno machache kutoka kwa Biblia?” Osman akakubali.

Walipokuwa wakielekea kwenye kaburi, Osman aliuliza maswali kadhaa kuhusu yule aliyekufa na akafikiria baadhi ya maandiko ambayo angetumia. Baada ya kufika kaburini, alijitambulisha kwa umati na kuwaeleza kwamba akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, anashiriki katika kazi ya kuwahubiria watu habari njema.

Kisha akitumia Ufunuo 21:3, 4 na Yohana 5:28, 29, akafafanua kwamba Mungu hakukusudia kamwe wanadamu wafe. Aliwaeleza kwamba hivi karibuni Mungu atawafufua wale waliokufa, nao watakuwa na tumaini la kuishi milele hapa duniani. Baada ya Osman kumaliza, wengi walimkumbatia na kumshukuru kutoka moyoni kwa sababu ya “habari njema kutoka kwa Yehova.” Kisha akarudi kwenye kigari cha machapisho.

Baada ya mazishi, baadhi ya waombolezaji walikuja kwenye kigari cha machapisho na kumuuliza Osman na familia yake maswali kuhusu Biblia. Wakawa na mazungumzo marefu, kisha wakachukua karibu machapisho yote yaliyokuwa kwenye kigari.