Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Uswisi

Uchunguzi uliofanywa nchini Uswisi unaonyesha kwamba kuna uwezekano wa asilimia 14 zaidi wa mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 60 kufa kwenye siku aliyozaliwa kuliko siku nyingine. Katika siku ya kuzaliwa, uwezekano wa kufa kutokana na mshtuko wa moyo huongezeka kwa asilimia 18 zaidi kuliko siku nyingine, uwezekano wa wanawake kupatwa na kiharusi huongezeka kwa asilimia 21, na uwezekano wa wanaume kujiua huongezeka kwa asilimia 35. Wanasayansi wanadhani kwamba mkazo na kileo vinachangia ongezeko la visa vya kujiua na aksidenti. Hata hivyo, wataalamu fulani hawakubaliani na uchunguzi huo, wakisema kwamba watu walioandika tarehe hizo ndio waliokosea na kufanya ionekane kwamba watu walikufa tarehe sawa na ile waliyozaliwa.

Israel

Kuna uwezekano mkubwa wa wanaume wenye sura nzuri kuitwa kwenye mahojiano ya kazi wanapoambatisha picha yao pamoja na maombi yao; lakini kwa wanawake warembo mambo ni tofauti. Kwa nini? Watafiti nchini Israel wanasema kwamba wafanyakazi wengi katika idara zinazoshughulikia ajira—zenye jukumu la kuamua ni nani atakayeitwa kwa ajili ya mahojiano—ni wanawake. Gazeti The Economist linasema sababu iliyotolewa ni kwamba “wivu uliwafanya wanawake hao wawabague wanawake warembo waliotuma maombi ya kazi.”

Marekani

Watu watatu wanaopinga vikali mambo ya vita—mtawa wa kike mwenye umri wa miaka 82 pamoja na wanaume wawili wenye umri wa miaka 63 na 57—hivi karibuni walifaulu kuingia eneo lenye ulinzi mkali la Oak Ridge, Tennessee, linalohifadhi tani 100 za vifaa vya nyuklia, na kuchora maandishi ya kupinga vita kwenye ukuta wa jengo moja. Kuzorota kwa usalama kwenye mojawapo ya maeneo “yanayopaswa kuwa na ulinzi mkali zaidi duniani . . . ni jambo linalozua wasiwasi sana,” anasema Waziri wa Nishati Steven Chu.

Australia

Mahakama ya juu zaidi nchini humo inataka makampuni ya sigara yaondoe rangi za pekee na nembo kwenye pakiti za sigara. Sasa, sigara zote zinapaswa kuuzwa katika pakiti za rangi nzito ya kahawia zikiwa na michoro yenye kutisha inayoonyesha hatari za uvutaji wa sigara.