Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kidingapopo—Tisho Linaloongezeka

Kidingapopo—Tisho Linaloongezeka

Kidingapopo​—Tisho Linaloongezeka

“Huduma za Afya za Morelos . . . , kwa ushirikiano na Kamati ya Afya ya Baraza la Mji wa Emiliano Zapata, wanalituza Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova cheti . . . kwa sababu ya ushirikiano [wa Mashahidi] kwa kufaulu kudumisha mazingira safi ili mbu wanaoambukiza ugonjwa wa kidingapopo wasiweze kuzaana.”

MAOFISA wa afya nchini Mexico wana sababu nzuri ya kuhangaika kuhusu mbu wanaoambukiza magonjwa. Wadudu hawa wadogo na wasumbufu wanaweza kuambukiza virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa kidingapopo ambao uliathiri zaidi ya watu 57,000 nchini Mexico katika mwaka wa 2010. Mexico ni moja tu kati ya nchi zaidi ya 100 ambako kwa sasa ugonjwa wa kidingapopo umeenea. Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linakadiria kwamba kila mwaka, huenda visa zaidi ya milioni 50 vya maambukizo ya kidingapopo hutukia ulimwenguni pote, na kwamba angalau watu wawili kati ya watano ulimwenguni pote wamo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo. Kupatana na hilo, maofisa wa afya wameanzisha programu za kuangamiza mbu mwenye madoadoa meupe anayeitwa Aedes aegypti, mmoja wa wadudu wanaoambukiza virusi vya kidingapopo. *

Kidingapopo huenea sana katika maeneo yenye joto na yale yenye joto la kadiri, hasa katika majira ya mvua na baada ya misiba ya asili kama kimbunga au mafuriko. Hii ni kwa sababu mbu anayeitwa Aedes wa kike hutaga mayai yake mahali palipo na maji ambayo hayasongi. * Kwa kuwa watu katika Amerika ya Latini na ya Karibea hukusanya na kuhifadhi maji ndani ya matangi yaliyotengenezwa kwa saruji, wataalamu wa afya wanawasihi wafunike matangi hayo. Hilo huzuia matangi hayo yasiwe maeneo ya mbu ya kutagia mayai. Pia, watu wanaweza kudhibiti kuenea kwa mbu hao wanapodumisha ua ukiwa safi kwa kuondoa magurudumu ya gari ya zamani, mikebe, nyungu za maua, vyombo vya plastiki—chochote kinachoweza kuzuia maji yasisonge.

Kutambua na Kukabiliana na Kidingapopo

Si rahisi kutambua ugonjwa wa kidingapopo kwa sababu dalili zake hufanana sana na zile za homa. Lakini kulingana na WHO, unapaswa kushuku kwamba una kidingapopo mara tu unapoona dalili za homa inayoandamana na kutokwa na vipele kwenye ngozi, maumivu nyuma ya macho, kwenye misuli, au maumivu makali ya viungo. Homa hiyo huendelea kwa siku tano hadi saba.

Madaktari bado hawana tiba ya kidingapopo, lakini mara nyingi ugonjwa huo unaweza kutibiwa nyumbani kwa kupumzika na kunywa vinywaji vingi. Hata hivyo, ni muhimu wagonjwa wachunguzwe vizuri kwa kuwa wanaweza kuanza kuvuja damu au kupatwa na mshutuko unaotokezwa na ugonjwa huo. Hali hizo hatari hutokea baada ya homa kuanza kupungua na huenda mgonjwa akaonekana kuwa anapata nafuu. Ni nini dalili za hali hizo hatari? Maumivu makali ya tumbo, kutapika sana, kutokwa na damu kwenye pua na kwenye fizi, kinyesi cha rangi nyeusi, na malengelenge ya rangi ya zambarau kwenye ngozi. Zaidi ya hayo, dalili ya mshtuko wa kidingapopo zinaweza kutia ndani kutotulia, kiu isiyo ya kawaida, ngozi kugeuka rangi na kuwa baridi, na shinikizo la chini sana la damu.

Inasikitisha kwamba dawa za kutibu magonjwa yanayosababishwa na viini, au bakteria (antibiotics) haziwezi kutibu ugonjwa wa kidingapopo kwa sababu unasababishwa na virusi wala si bakteria. Ni jambo la hekima pia mgonjwa aepuke dawa za kupunguza maumivu kama vile aspirini na ibuprofen kwa sababu zinaweza kuongeza hatari ya kuanza kuvuja damu. Kuna aina nne za virusi vinavyoambukiza ugonjwa wa kidingapopo, na inawezekana kuambukizwa ugonjwa huo zaidi ya mara moja.

Ukipatwa na kidingapopo, pumzika vizuri na unywe vinywaji vingi. Pia, lala ndani ya neti ya mbu kadiri inavyowezekana ili uzuie mbu wasikuume na kuwaambukiza wengine ugonjwa huo.

Unaweza kufanya nini ili uepuke kuumwa na mbu? Vaa shati lenye mikono mirefu, suruali au rinda refu, na utumie dawa za kufukuza mbu. Ingawa mbu wanaweza kuuma wakati wowote, wao huwa wengi sana saa mbili kabla ya jua kutua na baada ya jua kuchomoza. Pia, kulala ndani ya neti yenye dawa inayofukuza mbu ni kinga.

Jitihada zinafanywa ili kutafuta chanjo ya kuzuia kidingapopo. Hatimaye, Ufalme wa Mungu utaondoa magonjwa yote, kutia ndani homa hiyo. Kwa kweli, wakati utafika ambapo Mungu “atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.”—Ufunuo 21:3, 4.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Katika nchi fulani, mbu wa aina nyingine, kama vile Aedes albopictus, pia huenda akabeba virusi vya kidingapopo.

^ fu. 4 Mbu aina ya Aedes hawaendi mbali sana na mahali walipoanguliwa.

[Mchoro katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Hakikisha Hakuna Maeneo Ambayo Mbu Wanaweza Kutaga Mayai

1. Magurudumu yaliyotupwa

2. Michirizi ya maji ya mvua

3. Nyungu za maua

4. Vyombo vya plastiki

5. Mapipa na mikebe iliyotupwa

Usikae Mahali Palipo na Mbu Wengi

a. Vaa shati lenye mikono mirefu, suruali au rinda refu. Tumia dawa za kufukuza mbu

b. Lala ndani ya neti

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Source: Courtesy Marcos Teixeira de Freitas