Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hulda Alifikia Lengo Lake

Hulda Alifikia Lengo Lake

IKIWA ungetembelea kisiwa kidogo cha Sangir Besar nchini Indonesia miaka kadhaa iliyopitia, huenda ungewaona dada watatu Wakristo ufuoni. Wanajulikana sana kisiwani humo kwa sababu ya huduma yao, yaani, ya kuwasaidia watu waielewe Biblia. Lakini katika pindi hiyo, walikuwa wakifanya kazi tofauti.

Kisiwa cha Sangir Besar kilicho kaskazini mwa Indonesia

Kwanza, wangeingia baharini na kutoa mawe makubwa huko na kuyapeleka ufuoni. Baadhi ya mawe yalikuwa na ukubwa kama wa mpira wa miguu. Kisha, wanawake hao waliketi kwenye viti vidogo vya mbao na kwa kutumia nyundo wakavunja-vunja mawe hayo katika vipande vilivyo vidogo kuliko yai la kuku. Baada ya hapo, waliyaweka mawe hayo madogo kwenye ndoo za plastiki, waliyabeba na kuyapeleka juu mahali walipokuwa wakiishi. Kisha waliweka mawe hayo kwenye mifuko mikubwa ambayo ingeweza kubebwa na malori na yalitumiwa kwenye ujenzi wa barabara.

Hulda, akikusanya mawe ufuoni

Mmoja wa dada hao anaitwa Hulda. Hali zake zilimruhusu kutumia muda mwingi zaidi kuliko wale wengine kufanya kazi hiyo. Kwa kawaida anatumia pesa anazopata ili kununua mahitaji ya familia ya kila siku. Lakini wakati huu alitaka kutunza kiasi fulani cha pesa hizo kwa ajili ya jambo lingine. Alitaka kununua tablet ili aweze kutumia programu ya JW Library®. Hulda alijua kwamba video na mambo mengine yaliyokuwa kwenye programu hiyo yangeboresha huduma yake na uelewaji wake wa Biblia.

Hulda alifanya kazi kwa saa mbili zaidi kila asubuhi, kwa mwezi mmoja na nusu, na akaweza kuvunja mawe ya kutosha kujaza lori ndogo. Hatimaye, aliweza kupata pesa za kutosha kununua tablet.

Hulda akiwa na tablet yake

Hulda alisema hivi, “Ingawa nilichoka kimwili na nilikuwa na maumivu kwa sababu ya kuvunja mawe, muda mfupi baadaye nilisahau maumivu hayo nilipopata tablet yangu mpya iliyonisaidia kuwa mwenye matokeo zaidi katika huduma na kujitayarisha kwa urahisi zaidi na mikutano ya Kikristo.” Pia, alisema kwamba tablet hiyo ilimsaidia kujiunga na wengine kwa ajili ya mikutano ya kutaniko na kuhubiri wakati wa janga la COVID-19. Tunafurahi kwamba Hulda alifikia lengo lake.