Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

TUNAJIFUNZA NINI KUTOKANA NA HISTORIA

Ignaz Semmelweis

Ignaz Semmelweis

IGNAZ SEMMELWEIS hajulikani sana, hata hivyo, kazi yake imenufaisha watu wengi leo. Ignaz alizaliwa Buda (sasa Budapest) nchini Hungaria, na akatunukiwa shahada ya Udaktari katika Chuo kikuu cha Vienna mwaka wa 1844. Baada ya kuchaguliwa kuwa profesa msaidizi katika Kliniki ya Kwanza ya Uzazi ya Hospitali Kuu ya Vienna mwaka wa 1846, Semmelweis alijionea hali mbaya sana, yaani, zaidi ya asilimia 13 ya wanawake walikufa kutokana na maradhi waliyoambukizwa wakati wa kujifungua, ugonjwa unaoitwa childbed fever.

Watu walikuwa na maoni mbalimbali kuhusu chanzo cha maradhi hayo, lakini hakuna ufumbuzi uliopatikana. Wengi walijaribu kutafuta suluhisho lakini jitihada zao hazikufanikiwa. Semmelweis aliumia sana kuwaona wanawake wengi wakifa kwa maumivu naye aliazimia kutafuta chanzo na kinga ya maradhi hayo.

Hospitali ambayo Semmelweis alifanya kazi ilikuwa na wodi mbili za wazazi, na kwa kushangaza idadi ya vifo katika wodi moja ilikuwa ya juu kuliko nyingine. Tofauti ya wodi hizo ni kwamba wanafunzi wa tiba walifundishwa katika wodi ya kwanza, na wakunga katika wodi ya pili. Kwa nini idadi ya vifo ilitofautiana katika wodi hizo mbili? Semmelweis alianza kuchunguza mambo ambayo huenda yalisababisha maradhi hayo, lakini hakufaulu.

Mwanzoni mwa mwaka wa 1847, Semmelweis alipata habari muhimu sana. Jakob Kolletschka, rafiki na mfanyakazi mwenzake alikufa baada ya kuambukizwa maradhi alipokuwa akifanyia uchunguzi maiti. Aliposoma ripoti kuhusu kifo cha Kolletschka, alitambua kwamba kilifanana kwa njia fulani na cha wanawake waliokufa baada ya kujifungua. Kwa hiyo, Semmelweis alihisi kwamba huenda “sumu” kutoka kwenye maiti ilieneza magonjwa kwa wanawake wajawazito na hivyo kusababisha maradhi hayo. Madaktari na wanafunzi ambao walifanyia uchunguzi maiti na kisha kuingia kwenye wodi ya wazazi walieneza maradhi bila kujua kwa wajawazito kabla au wakati wa kujifungua! Idadi ya vifo kwenye wodi ya pili ilikuwa dogo kwa sababu wakunga hawakufanyia uchunguzi maiti.

Mara moja, Semmelweis alianzisha sera mpya ya kunawa mikono kwa dawa ya kuua vijidudu kabla ya kuwahudumia wanawake wajawazito. Kulikuwa na matokeo mazuri: idadi ya vifo ilipungua kutoka asilimia 18.27 mwezi wa Aprili hadi 0.19 kufikia mwisho wa mwaka huo.

“Ugunduzi wangu umekusudia kumaliza vifo katika wodi za wazazi, kuokoa uhai wa mke kwa ajili ya mume wake na mama kwa mtoto wake.”—Ignaz Semmelweis

Watu wengi hawakupendezwa na ugunduzi wa Semmelweis. Matokeo ya uchunguzi wake kuhusu viini vya maradhi yaliyosababisha vifo vya wanawake baada ya kujifungua yalipingana na nadharia za wataalamu wengine ambao pia walipinga sera yake mpya ya kunawa mikono. Baadaye, Semmelweis alifutwa kazi huko Vienna na hivyo akarudi nchini Hungaria. Akiwa Pest nchini Hungaria, alifanya kazi akiwa msimamizi wa idara ya wakunga katika Hospitali ya St. Rochus ambako sera yake ilisaidia kupunguza idadi ya vifo kufikia chini ya asilimia moja.

Mwaka wa 1861, Semmelweis alichapisha kitabu chake kiitwacho, The Cause, Concept, and Prophylaxis of Childbed Fever. Kwa kusikitisha, ugunduzi wake haukuthaminiwa hadi miaka mingi baadaye. Kwa sababu ya kupuuza ushauri wake, watu wengi walikufa katika kipindi hicho.

Semmelweis alisisitiza kunawa mikono katika vituo vya afya alivyokuwa akisimamia.—Painting by Robert Thom

Baadaye, Semmelweis aliheshimiwa kwa kuwa mvumbuzi wa mbinu ya kuua viini inayotumika sasa. Ugunduzi wake ulichangia kuelewa kwamba viini vinaweza kusababisha magonjwa. Pia, alichangia sehemu kubwa katika uvumbuzi wa viini vya maradhi ambao huonwa kuwa “mchango muhimu sana katika sayansi ya tiba.” Kwa kupendeza, zaidi ya miaka 3,000 iliyopita, Sheria ya Musa ambayo baadaye iliandikwa katika Biblia, ilitoa mwongozo unaofaa kuhusu jinsi ya kushughulikia maiti.