Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa Kunusa wa Mbwa

Uwezo wa Kunusa wa Mbwa

 Watafiti wanasema kwamba mbwa wanaweza kutambua umri, jinsia, na hali ya kihisia ya mbwa wengine kwa kutumia uwezo wao wa kunusa. Mbwa wanaweza hata kuzoezwa kutambua mabomu au dawa za kulevya. Ingawa wanadamu hutumia hasa uwezo wao wa kuona kuchunguza mazingira, mbwa hutumia uwezo wao wa kunusa.

 Jambo la kufikiria: Uwezo wa kunusa wa mbwa ni bora mara elfu kadhaa ukilinganishwa na wetu. Kulingana na Taasisi ya Marekani ya Viwango na Teknolojia, mbwa “anaweza kunusa kemikali fulani kwa viwango vidogo sana, yaani, sehemu iliyogawanywa mara trilioni. Uwezo huo ni kama kuonja ladha ya sukari inayolingana na robo ya kijiko cha chai iliyoyeyushwa katika kidimbwi cha kuogelea chenye ukubwa wa uwanja wa Olimpiki.”

 Ni nini kinachofanya mbwa awe na uwezo mkubwa hivyo wa kunusa?

  •   Pua ya mbwa ina unyevunyevu kwa hiyo, inaweza kunasa harufu kwa urahisi zaidi.

  •   Pua ya mbwa imejigawa mara mbili​—njia moja ni ya kupumulia, nyingine ya kunusa. Mbwa anaponusa, hewa inaelekezwa upande wa pua wenye vipokezi vya kutambua harufu.

  •   Sehemu ya pua ya mbwa iliyotengwa kwa ajili ya kunusa inaweza kuwa na ukubwa wa sentimita 130 za mraba au zaidi, ilhali sehemu hiyo kwenye pua ya mwanadamu ni sentimita 5 tu za mraba.

  •   Idadi ya chembe za kutambua harufu za mbwa inaweza kuwa mara 50 ukilinganisha na zetu.

 Hayo yote yanamsaidia mbwa kutofautisha sehemu mbalimbali zinazofanyiza harufu fulani. Kwa mfano, wataalamu fulani wanasema kwamba wanadamu wanaweza kunusa supu, lakini mbwa anaweza kunusa kila kiungo kwenye supu hiyo.

 Watafiti wa Taasisi ya Pine Street, ambayo inashughulikia utafiti kuhusu kansa, wanasema kwamba ubongo na pua ya mbwa zinapofanya kazi pamoja zinafanyiza “mojawapo ya vifaa tata zaidi vya kutambua harufu duniani.” Wanasayansi wanajitahidi kubuni “pua” ya kielektroni inayoweza kutambua kuwepo kwa mabomu, dawa za kulevya, na magonjwa, kutia ndani kansa.

 Una maoni gani? Je, uwezo wa mbwa wa kunusa ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?