Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa Popo Kutambua Vitu Vilipo kwa Kutumia Mwangwi

Uwezo wa Popo Kutambua Vitu Vilipo kwa Kutumia Mwangwi

 Ingawa wana uwezo wa kuona, aina nyingi za popo hutumia mwangwi kutambua mazingira yao wanaporuka usiku. Hilo linamaanisha kwamba wanatambua umbali wa kitu kwa kutegemea muda ambao sauti itawarudia. Kwa mfano, popo fulani wanaweza kutofautisha kati ya mbu na mbawakawa kwa kusikiliza mapigo ya mabawa ya wadudu hao.

 Fikiria hili: Popo wengi hutokeza sauti katika zoloto na kuzitoa kupitia mdomo au pua zao. Kisha wanatumia masikio yao makubwa kutambua mwangwi wowote unaotokea baada ya mawimbi ya sauti kugonga kitu fulani. Mwangwi huo humwezesha popo kupiga picha akilini ya mazingira yake yote. Popo anaweza kutambua mahali, mwinuko, na umbali wa kitu, hata ikiwa kuna kelele nyingi zinazotokezwa na popo wengine.

 Popo anahitaji kuwa sahihi kabisa anapotambua vitu vilipo kwa sababu kukosea hata kwa chini ya nusu sekunde kunaweza kumfanya akose shabaha yake kwa sentimita 17. Kulingana watafiti fulani, kulenga shabaha kwa usahihi kabisa wa chini ya nusu sekunde “ni jambo linaloonekana kuwa haliwezekani.” Hata hivyo, majaribio yaliyofanywa yanaonyesha kwamba popo wana uwezo wa kutoa mwangwi kwa usahihi kabisa wa muda wa mara 100,000,000 ya sekunde (10 nanoseconds) jambo linalowawezesha kukadiria umbali kwa usahihi wa milimita moja au hata chini ya hapo!

 Watafiti wametengeneza fimbo ya umeme inayotumia mwangwi kutambua vitu vilipo ili kuwasaidia vipofu kupata picha akilini ya mazingira yao na kuwawezesha kuepuka vikwazo, kutia ndani vile ambavyo viko juu kama tawi la mti. Brian Hoyle na Dean Waters, ambao ni wawili kati ya wataalamu waliobuni fimbo hiyo ya umeme inayoitwa Batcane, wanasema hivi: “Tulichochewa kuitengeneza hasa baada ya kutambua uwezo wenye kustaajabisha wa popo kutambua vitu vilipo kwa kutumia mwangwi.”

 Una maoni gani? Je, uwezo wenye kustaajabisha wa popo kutambua vitu vilipo kwa kutumia mwangwi ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?