Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Gundi ya Kiganzimwamba

Gundi ya Kiganzimwamba

 Kwa muda mrefu wanazuolojia wameona uwezo mkubwa wa kiganzimwamba wa kujishikiza kwa nguvu kwenye mawe, gati, na mashua. Gundi ya kiganzimwamba inasemekana kuwa bora zaidi kuliko gundi yoyote iliyotengenezwa na wanadamu. Hadi hivi karibuni, wanadamu hawakuelewa jinsi kiganzimwamba anavyojigandisha kwenye sehemu zenye umajimaji.

 Jambo la Kufikiria: Uchunguzi unaonyesha kwamba kiganzimwamba akiwa buu huogelea huku na huku akitafuta sehemu nzuri ambapo ataweza kujishikiza. Mara anapopata sehemu nzuri ya kuishi, anatoa aina mbili za umajimaji. Moja ni mafuta ambayo huondoa maji kwenye sehemu aliyochagua kunata. Pia mafuta hayo huandaa mazingira mazuri kwa ajili ya aina ya pili ya umajimaji ambao umefanyizwa na protini zinazoitwa phosphoproteins.

 Kwa pamoja, aina hizo mbili za umajimaji hutengeneza gundi imara inayoitwa plaque ambayo haimomonyolewi hata na bakteria. Ni muhimu sana gundi yake iendelee kuwa imara kwa kuwa kiganzimwamba huishi maisha yake yote akiwa amenata kwenye sehemu hiyo.

Viganzimwamba, picha ndogo inaonyesha nyuzinyuzi za gundi yake

 Gundi ya kiganzimwamba hutengenezwa kwa njia tata kuliko ilivyofikiriwa awali. Mmoja wa wataalamu waliogundua jinsi gundi hiyo inavyotengenezwa alisema hivi: “Hii ni njia yenye kustaajabisha sana ya kiasili ya kushughulika na changamoto ya kugundisha vitu vyenye umajimaji.” Huenda uvumbuzi huo ukawasaidia watafiti kutengeneza gundi ambayo itafaa kutumika majini, na pia kutokeza gundi za asili zitakazotumiwa kwenye vifaa vya kielektroni na viungo bandia.

 Una maoni gani? Je, gundi ya kiganzimwamba ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?