Hamia kwenye habari

Heather Broccard-Bell/iStock via Getty Images

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Gamba la Mbawakawa Anayeitwa “Diabolical Ironclad”

Gamba la Mbawakawa Anayeitwa “Diabolical Ironclad”

 Mbawakawa anayeitwa diabolical ironclad (Phloeodes diabolicus) anaishi katika upande wa magharibi wa Amerika Kaskazini. Kulingana na watafiti, mbawakawa huyo anaweza kuhimili uzito unaozidi ule wa mwili wake kwa mara 39,000 na anaweza hata kupona anapokanyagwa na gari. Mbawakawa huyo anawezaje kuhimili shinikizo kubwa hivyo?

 Sehemu za juu na za chini za gamba la mbawakawa huyo huungana kwenye sehemu zilizo na nyufa. Aina moja ya nyufa hizo haiwezi kubonyea inapogandamizwa, na hivyo kulinda viungo muhimu. Aina nyingine inaweza kuruhusu gandamizo. Na aina ya tatu ya nyufa hizo huruhusu sehemu ya juu ya gamba lake kusogea. Unyumbulikaji wa aina hiyo ya tatu huruhusu mdudu huyo kupenya ndani ya gamba la mti au kujificha kwenye mianya midogo sana kwenye mwamba.

 Mbali na hilo, mshono ulio katikati ya gamba la mbawakawa huyo una ncha kadhaa zinazoungana kama meno ya zipu na hivyo uzito haugandamizi sehemu moja ya mwili wake bali unaenezwa. Ncha hizo zimefanyizwa kwa matabaka yaliyounganishwa kwa protini. Protini hizo zinapogandamizwa, zinasababisha mipasuko midogo ambayo hatimaye hupona na kuruhusu ncha hizo kuhimili shinikizo bila kutengana.

Ncha huungana kama meno ya zipu

Kishale chekundu kinaonyesha nyufa zinazounga sehemu ya juu na ya chini ya gamba la mbawakawa huyo. Kishale cha kijivu kinaonyesha ncha zinazoungana kwenye mshono ulio katikati ya gamba hilo

 Watafiti wanasema kwamba wataalamu wanaweza kuiga gamba la mbawakawa huyo wanapobuni vitu vinavyohitaji kuhimili shinikizo au mgandamizo, kama vile magari, madaraja, na majengo.

 Una maoni gani? Je, gamba la mbawakawa anayeitwa diabolical ironclad lilijitokeza lenyewe? Au lilibuniwa?