Hamia kwenye habari

BluePlanetArchive/Whale Watch Azores

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Nyangumi Aina ya Cuvier, Mpiga Mbizi Hodari

Nyangumi Aina ya Cuvier, Mpiga Mbizi Hodari

 Nyangumi aina ya Cuvier ambaye pia huitwa nyangumi domo refu wa Cuvier, anaweza kupiga mbizi hadi kufikia kina cha mita 2,992 katika maji yenye shinikizo la kilopaskali 30,300. Nyangumi huyo anaweza kukaa chini ya maji kwa muda mrefu. Katika utafiti mmoja, nyangumi huyo alikaa chini ya maji kwa saa 3 na dakika 42 kabla ya kurudi juu ili kupumua. Nyangumi ni wa familia ya mamalia kwa hiyo wanahitaji kuja juu ya maji ili kupumua, basi ni nini kinachowasaidia kustahimili shinikizo kali la maji na kutumia oksijeni kidogo kwa muda mrefu?

 Kama tu mamalia wengine wanaoishi ndani ya maji, mbavu zake zinajikunja na oksijeni inatoka kwenye mapafu hivyo basi ukubwa wa mapafu unapungua. Watafiti wamegundua kwamba mamalia wanaoishi ndani ya maji wanatumia oksijeni kidogo wanapokuwa chini ya maji kwa sababu mapigo ya moyo wao yanapungua sana na damu kutoka sehemu nyingine za mwili wao inaelekezwa kwenye ubongo, moyo, na misuli.

 Isitoshe, mamalia hao huhifadhi oksijeni katika misuli yao kwa msaada wa protini inayoitwa mayoglobini. Vilevile, wanapopiga mbizi kwenye maji yenye kina kirefu, mayoglobini inatoa oksijeni hatua kwa hatua kadiri inavyohitajika. Misuli yao ina kiwango kikubwa zaidi cha mayoglobini kwa kulinganisha na misuli ya wanadamu na ya wanyama wa nchi kavu.

 Hata hivyo, mtafiti mmoja alisema hivi kuwahusu nyangumi aina ya Cuvier: “Nyangumi hawa wanapopiga mbizi wanafikia kina cha kustaajabisha. Kulingana na ujuzi tulio nao kuhusu fiziolojia, nyangumi hawa wanapopiga mbizi wanafikia kina kirefu sana na pia wanabaki chini ya maji muda mrefu zaidi kuliko vile ambavyo tungetazamia.” Wanasayansi wanajitahidi kuelewa vizuri zaidi uwezo wa nyangumi wa kupiga mbizi ili kuboresha matibabu wanayotoa kwa ajili ya matatizo ya mapafu na hasa mapafu yaliyofungana.

 Una maoni gani? Je, uwezo wa nyangumi aina ya Cuvier wa kupiga mbizi kufikia kina kirefu na kubaki humo kwa muda mrefu ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?